TUSALI SALA YA ASUBUHI
TUSALI SALA YA ASUBUHI
+Kwajina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
Tuusifu Utatu Mtakatifu wa Mungu mmoja, sasa na siku zote na
milele amina. Ee utatu Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu; +Baba, +Mwana na +Roho
Mtakatifu. Ninasadiki kuwa upo hapa na mahali pote.
Ee Mungu wangu, umeniumba, umenikomboa, umenifanya mkristu,
umenizidishia neema zako, umenitayarishia makao yangu mbinguni.
Ee Mungu wangu, nakuabudu, nakushukuru, nakuomba toba,
nakupenda. Ee Mungu wangu, ninakutolea roho yangu, na mawazo, na maneno, na
kazi na furaha, na mateso yangu, uyapokee unipe neema yako nisitende leo
dhambi, Amina.
______________________
Ee Baba yetu Mungu mkuu,
Umenilinda usiku huu.
Nakushukuru kwa moyo,
Ee Baba, Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii,
Niache dhambi, nikutii.
Naomba sana Baba wee,
Baraka zako nipokee.
Bikira safi, Ee Maria
Nisipotee nisimamie.
Mlinzi mkuu malaika wee,
Kwa Mungu wetu niombee
Nitake nitende mema tu,
Na mwisho nije kwako juu. Amina.
NIA NJEMA.
Kumheshimu Mungu wangu
Namtolea roho yangu,
Nifanye kazi nipumzike
Amri zake tu nishike
Wazo, neno, tendo lote
Namtolea Mungu pote
Roho, mwili chote changu,
Pendo na uzima wangu
Mungu wangu nitampenda,
Wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,
Utakalo hutimia.
Kwa utii navumilia
Teso na matata pia.
Nipe, Bwana, neema zako
Niongeze sifa yako. Amina.
•SALA YA MATOLEO.
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka
yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha zangu zote za leo. Ee
Yesu, ufalme wako utufikie.
BABA YETU.
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako
ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama
tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini
utuopoe maovuni. Amina.
SALAMU MARIA.
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko
wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na
saa ya kufa kwetu. Amina.
KANUNI YA IMANI.
Nasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi. Muumba wa Mbingu na dunia. Na
kwa Yesu Kristo Mwanae wa pekee, Bwana wetu. Aliyetungwa kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria. Akateswa kwa mamlaka ya Ponsiyo Pilato.
Akasulibiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu. Siku ya tatu akafufuka katika
wafu. Akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Toka huko atakuja
tena kuwahukumu wazima na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, kanisa takatifu katoliki, ushirika
wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo.
Amina.
AMRI ZA MUNGU.
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu Miungu wengine.
2. Usilitaje bure jina la Mungu wako.
3. Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini.
7. Usiibe.
8. Usiseme uongo.
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.
AMRI ZA KANISA.
1. Hudhuria misa takatifu, dominika na sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya jumatano ya majivu; usile nyama siku ya ijumaa
kuu.
3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi takatifu hasa wakati wa Paska.
5. Saidia kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.
Ee Maria Bikira Mtakatifu, Mama wa Mungu na Mama yangu, nawe
Mtakatifu Yosefu, Nawe malaika mlinzi wangu, nanyi watakatifu somo wangu, nanyi
watakatifu wote, niombeeni nipate kuacha dhambi, nilindeni siku ya leo na siku
zote, na saa ya kufa kwangu, Amina.
SALA YA IMANI.
Mungu wangu, nasadiki maneno yote. Linayosadiki na
linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma. Kwani ndiwe uliyetufumbulia hayo. Wala
hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina.
SALA YA MATUMAINI.
Mungu wangu, natumaini kwako, nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo.
Neema zako hapa duniani, na utukufu mbinguni. Kwani ndiwe uliye agana hayo
nasi, nawe mwamini. Amina.
SALA YA MAPENDO.
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote. Kwani ndiwe mwema,
ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu, kama nafsi yangu, kwa ajili
yako. Amina.
SALA YA KUTUBU.
Mungu wangu nimetubu sana, niliyokosa kwako. Kwani ndiwe mwema,
ndiwe nwenye kupendeza. Wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena.
Nitafanya kitubio, naomba neema yako, nipate kurudi. Amina.
SALA KWA MALAIKA
MLINZI.
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote, za roho na za
mwili. Amina.
MALAIKA WA BWANA
•Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria, Naye akapata mimba kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu.
~Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko
wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu mama wa
Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
•Ndimi mtumishi wa Bwana, Nitendewe ulivyosema.
~Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko
wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu mama wa
Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
•Neno wa Mungu akautwaa mwili, akakaa kwetu.
~Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko
wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu mama wa
Mungu, utuombee sisi wakosefu. Sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.
Utuombee Mzazi Mtakatifu wa Mungu, tujaliwe ahadi za Kristo.
Tuombe:
Tunakuomba Ee Bwana utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi
tuliojua kwa maelezo ya malaika, kwamba Kristo mwanao amejifanya mtu; kwa
mateso na msalaba wake, tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Tunaomba hayo kwa
njia ya Kristo Bwana wetu, Amina.
*SALA YA KUOMBA KUWA
MKARIMU*
■Bwana Yesu, nifundishe kuwa mkarimu;
■Nifundishe kukutumiki unavyostahili;
■Kutoa bila kuhesabu gharama;
■Kupigana bila kujali ujeruhi;
■Kujitahidi bila kutafuta pumziko;
■Kutumika bila kutafuta tuzo;
■Ispokuwa kule kujua nafanya mapenzi yako ......Amina
*SALA YA KUMSHUKURU
MUNGU*
Nakushukuru Ee Mungu kwa ulinzi na baraka zako zote
unazonijalia
Nakuomba unijalie hekima na busara katika kunena na katika
kutenda
unisaidie iliniweze kuyashinda maisha yanayo
nisongasonga. Nakuomba unisaidie niweze
kutimiza malengo yangu na unikinge hatari zote za mwili na za
roho katika kuyafikia malengohayo.Usiniache nianguke katika maovu. Uwape
mafanikio wote wanaohitaji msaada wako. Nakuomba unijalie kifo chema na
uwapokee kwako marehemu wote hasa ndugu zangu. Naomba haya yote kwa njia ya
Kristo Bwana wetu..... Amina.
*Sala kabla ya Kazi.*
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waumini wako uwatie mapendo
yako peleka roho wako vitaumbwa upya na nchi itageuka.
*Tuombe.*
Ee Mungu uliye fundisha nyoyo za waumini wako, ukiwaletea mwanga
wa Roho Mtatifu tunakuomba tuongozwe na yule Roho,tutende yaliyo mema tupate
daima na faraja zake.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. *Amina.*
*Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.Amina.*
Maoni
Chapisha Maoni