HISTORIA YA MAISHA YA BIKIRA MARIA
HISTORIA YA MAISHA YA BIKIRA MARIA
MAISHA
YA WAZAZI WA BIKIRA MARIA
Mnamo
karne ya pili kabla ya kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu kristo. Wazazi wa Bikira
Maria walijulikana katika Kanisa kwa majina ya JOAKIMU na ANNA. Hata ilipofika
karne ya nne, Wakristu wa kanisa la Mashariki walikuwa tayari wameshazoea
kuwaheshimu wazazi hawa. Mwaka 1548 Kanisa Katoliki lilianza rasmi kusherekea
sikukuu ya wazazi wa Mungu, Katika kalenda ya Kanisa sikukuu ya Watakatifu hawa
huadhimishwa tarehe 26 Julai kila mwaka.
BABA
MZAZI WA BIKIRA MARIA
Joakimu
ndiye Baba mzazi wa Bikira Maria, Baba huyu alikuwa wa kabila la Yuda na Ukoo
wa Mfalme Daudi. Jina Joakimu lina maana ya Matayarisho kwa ajili ya Bwana ; au Bwana anatayarisha. Mtakatifu
huyu aliishi Nazareti iliyoko Galilaya.
MAMA
MZAZI WA BIKIRA MARIA
Anna
ndiye mzazi wa Bikira Maria, Mama huyu alizaliwa katika ukoo wa Haruni Kuhani
Mkuu wa kabila la Yuda. Jina la Anna lina maana ya Neema au Enye Neema. Mama
huyu nyumbani kwao kulikuwa Betheremu mji wa Yerusalemu. Huko ndiko alikoishi
kabla ya kuolewa.
JOAKIMU
NA ANNA WACHA MUNGU HATA KABLA YA NDOA
Kutokana
na maasi ya wanadamu kwa Mungu wao, Nyakati hizo, kabla ya Joakimu na Anna
kufunga ndoa, Watu walikuwa wamechanganyikana katika makundi mawili, kwanza
kulikuwa na kundi la watu wacha Mungu na kundi la pili la watu wasiomcha Mungu.
Lakini
Joakimu alikuwa mcha Mungu sana na siku zote alisali akimuomba Mungu mambo
mawili, nayo ni mosi Masiha azaliwe ili aikomboe Dunia katika Maasi, pili
aliomba apate mke mwema na mcha Mungu kama yeye mwenyewe, Pia Anna alikuwa
msichana mcha Mungu sana, naye alisali kila siku akimuomba Mungu mambo mawili
vivyo hivyo kama Joakimu. Masiha aje mapema na apate Mume mcha Mungu kama yeye
mwenyewe. Ili waendeleze sala zao kwa pamoja wakiomba Mungu Masiha aje haraka
na kuikomboa dunia katika uasi na dhambi.
Wakati
Joakimu na Anna walipokuwa wakiomba hayo walikuwa hawafahamiani kabisa, wala
hawakujua kama siku moja watakuwa Mume na Mke. Kwani kila mmoja wao alikuwa
akisali nyumbani kwake. Joakimu akiwa Nazareti na Anna akiwa Betheremu. Lakini
kitu cha kushangaza na cha ajabu ni kwamba, kwanza sala zao na nia za maombi
yao zilifanana. Halafu saa au muda aliokuwa akisali kule kwake Nazareti hata
Anna naye alikuwa akisali kule kwao Betheremu.
MALAIKA
GABRIEL ANAWAPASHA HABARI ZA UCHUMBA.
Siku
zilipita nyingi Watakatifu hawa walidumu katika sala na kumtukuza Mungu. Na
kila waliposali hawakuacha kumweleza Mungu maombi yao hayo mawili, yaani Masiha aje haraka na kila mmoja wao apate mchumba ambaye ni
mcha Mungu. Basi mwisho Mungu akasikiliza sala na maombi yao; kama yasemavyo
maandiko Matakatifu, Ombeni mtapewa, tafuteni mtapata, pigeni hodi mtafunguliwa.
Math 7:7-11 ndivyo Mungu alivyofanya kwa Joakimu na Anna. Siku moja Mungu
alimtuma malaika Gabriel awapelekee ujumbe wa furaha kwa kila mmoja wao kwamba
watakuwa watu wa ndoa. (Mume na Mke).
Anna
alikuwa wa kwanza kutokewa na malaika Gabriel na kumwona kwa macho yake.
Malaika alipofika kwa Anna alimwambia. "Sala zako zimekubaliwa na
Mungu", Joakimu atakuwa Mume wako, usimkatae atakapofika kukutaka uchumba.
Na ndoa ikifungwa muendelee kusali mkimwomba Mungu bila kuchoka na Masiha
atazaliwa. Msichana huyu Mtakatifu licha ya kuwa mcha Mungu sana alikuwa na
sifa zingine nzuri.
Alikuwa
na sura nzuri ya kuvutia, bahati ya kujua na kujulishwa mambo mengi ya Mungu
kwa njia ya Malaika kuliko Joakimu. Baada ya Anna kujulishwa habari hizo,
ilipofika usiku wa siku hiyohiyo. Joakimu akiwa amelala usingizi mnono; Malaika
Gabriel alimtokea katika ndoto akamwambia "Anna atakuwa Mke wako nenda
kamchukue". Joakimu alipoamka asubuhi alifunga safari kwenda Betheremu
nyumbani kwao Anna. Akamchumbia na kufanya mipango ya ndoa. Siku chache baadaye
walifunga ndoa wakawa Mume na Mke.
MAISHA
YA NDOA NYUMBANI KWAO NAZARETI
Watakatifu
hawa baada ya kufunga ndoa yao walienda kuishi mjini Nazareti – Galilaya nyumbani
kwa Joakimu. Walidumu katika kumcha Mungu kwa sala, furaha na mapendo makubwa
ya ndoa yao. Licha ya kuwa na nyumba kule Nazareti – Galilaya walikuwa na
nyumba ndogo kule Yerusalem. Karibu na lango la ukuta wa Hekalu kuu. Kutoka
Nazareti mpaka Yerusalem ni umbali wa maili 68 au Km 109.5 kwa kutembea kwa
miguu, lakini kwa gari ni umbali wa maili 94.5 au Km 152.8 na ukitumia usafiri
wa ndege ni maili 63 au Km 101.4 Mungu aliwajalia na kuwabariki. Walikuwa na
utajiri mwingi wa Mali. Walikuwa na mashamba makubwa na mifugo mingi, kweli
walikuwa na kila kitu cha kuwafanya wawe na furaha duniani.
TABIA
ZAO
Joakimu
alipenda kufanya kazi ya kutunza mashamba na kuchunga mifugo yao kwenye milima
ya Galilaya. Naye Anna alipenda sana kumtunza mume wake na nyumba yao. Kwa
ujumla mama huyu alipenda sana kazi za nyumbani.
Kutokana
na mazao ya mashamba na mifugo yao walipouza walipata fedha nyingi. Na mapato
yao waliyatumia katika sehemu tatu. Kwanza
waliwagawia masikini, Pili walitoa
zaka na sadaka Hekaluni na Tatu
walitunza kwa ajili ya chakula chao na mahitaji mengine.
JOAKIMU
NA ANNA WANAKASHIFIWA NA MAJIRANI
Katika
miaka ishirini (20) waliyoishi ya Ndoa yao yenye kupendeza na kuvutia na kuwa
mfano wa kuigwa na jirani zao, Mungu hakuwajalia kupata mtoto hata mmoja. Hali
hii wao wenyewe walijisikia wanyonge na wakiwa sana; kwa kukosa mtoto wa
kuwachangamsha. Zaidi sana kutokana na kabila la Kiebrania, familia isiyokuwa
na mtoto hudhaniwa kuwa haina Baraka za Mungu. Hivyo watu walioishi nao jirani
waliwadharau sana na kuwatukana, kwa kuwakashifu kwamba walikuwa wagumba na
hawakuwa na thamani kwa Mungu. Hata Masiha akija walifikiri kwamba
hawatakombolewa.
Lakini
pamoja na kashifa zote hizo na kudharauliwa namna hiyo wao hawakujali, ila
walimshukuru Mungu na kumwomba sana awajalie kupata mtoto ili waweze kupumzika
na dharau na matusi ya watu; hasa ya jirani zao. Katika kuomba kwao Mungu awape
mtoto, Joakimu na Anna walimwahidi Mungu kuwa wakipata mtoto huyo awe wa kiume
au wa kike watamtolea kwake Mungu ili awe mtumishi wake Hekaluni. Waliamini pia
kuwa maombi na dua zao Mungu atazipokea na siku moja atawatendea mambo makuu ya
ajabu, mpaka jirani zao wataaibika. Kama tusomavyo katika "Yeremia 33:3, 9
Niite, name nitakuitikia, name nitakuonesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua. Na
mji huu utakuwa kwangu jina la furaha, na sifa na utukufu, mbele ya mataifa
yote ya dunia, watakaposikia habari ya mema yote niwatendeayo, nao wataogopa na
kutetemeka, kwa sababu ya mema yote na Amani nitakayoupatia mji huo."
JOAKIMU
ANAFUKUZWA HEKALUNI
Siku
moja Joakimu na jamaa zake walienda Hekaluni kusali na kutoa sadaka kwa ajili
ya kumuomba Mungu Masiha aje haraka pia kumwomba Mungu awajalie Joakimu na Anna
kupata mtoto. Lakini ilitokea humo Hekaluni mambo ya ajabu ambayo Joakimu na
jamaa zake yaliwastaajabisha na kuwatia uchungu sana.
Kwani
Joakimu alipambana na kuhani msaidizi aliyejulikana kwa jina la Isaack ambaye
alikuwa anawafahamu Joakimu na mke wake Anna kuwa ni matajiri wa Mali na mifugo
pia ni wacha Mungu lakini hawakuwa na mtoto hata mmoja. Yule Kuhani alimwendea
Joakimu mahali alipokuwa ameketi humo Hekaluni wakisali yeye na jamaa zake,
akamnyanyasa kwa kumwambia.
"WEWE
JOAKIMU KWANINI UMEKUJA HAPA KUMCHUKIZA MUNGU, WEWE HUNA MTOTO HATA MMOJA
UNAKUJA KUFANYA NINI? TOKA HUMU HEKALUNI UENDE ZAKO. HUJUI KUWA HIZO SALA NA
SADAKA ZAKO HAZINA THAMANI MBELE ZA MUNGU? WEWE NI MGUMBA, MTU USIYEFAA KABISA,
ONDOKA HUMU HEKALUNI SASA HIVI. USIZIDI KUMCHUKIZA MUNGU KWA HIZO SALA NA
SADAKA ZAKO."
Basi
Joakimu akiwa na aibu kubwa ya Moyo na mwili alifadhaika mno na akapata uchungu
mkali kwa maneno hayo. Kabla ya kuondoka humo Hekaluni baada ya kufukuzwa na
huyo Kuhani msaidizi alisujuduu na kumwomba Mungu akisema. "Mungu wangu
kwa amri na mapenzi yako nimekuja Hekaluni, lakini huyu aliyechukua nafasi yako
hekaluni ananinyanyasa, nami kutokana na dhambi zangu nastahili aibu hii. Basi
nakuomba Mungu wangu usinitupe mimi kiumbe chako dhaifu" mara baada ya
sala hiyo akaondoka haraka. Kutokana na aibu hiyo aliyoipata hakupenda hata
kurudi nyumbani kwake, bali aliondoka upesi akaenda moja kwa moja mpaka kwenye
mashamba yake ambako kulikuwa na ghala kubwa la kutunza mazao yao. Jamaa zake
aliwaacha humo humo hekaluni, ila yote aliyotendewa na huyo kuhani msaidizi
waliyashuhudia. Nao walisikia uchungu kuona jamaa yao alivyotendewa. Basi
Joakimu alipofika huko shambani akaingia ghalani akasali akasema.
"Mungu
wa Ibrahim, Mungu wa Yakobo, Mungu wa Isaack wewe umewasaidia vizazi na vizazi
na umetupa mwongozo wako ukisema yeyote atakayeomba kwa Imani utamsaidia. Mimi
sasa nakuomba kwa Imani. Nakuomba upokee sala zangu na za mwenzangu Anna. Utupe
mtoto. Na kama umetuona kuna kitu kinachozuia tusipate mtoto, tunakuomba sasa
ukiondoe. Ninazidi kukuahidi kuwa mtoto tutakayempata tutamtolea kwako awe
mtumishi wako Hekaluni".
Wakati
Joakimu anasali sala hiyo huko shambani, Anna mkewe kwa kipindi hicho hicho nae
alikuwa anasali nyumbani kwake. Aliomba Mungu awajalie kupata mtoto. Wala
hakujua mkasa uliokuwa umempata mume wake.
Sala aliyosali Anna ni hii.
"Mungu
wangu kumbuka wewe ulimpatia Anna somo yangu mtoto ambaye naye alikuwa Mgumba,
nakuomba kwa huruma yako na mapenzi yako unijalie na mimi kupata mtoto rejea (1
Samweli 1:1-20)"
MALAIKA
GABRIEL ANAWAPASHA HABARI NJEMA
Kilio
na sala za Watakatifu hawa zilimfurahisha Mungu. Hasa kwa jinsi walivyokuwa
wanyenyekevu wa moyo. Mara baada ya sala hizo Mungu alimtuma Malaika Gabriel
akamtokea Anna na kumjulisha kwamba sala zake zimepokelewa na Mungu, hivyo
atapata mtoto. Mama huyu aliposikia habari njema hiyo alijawa na furaha kubwa
sana isiyoelezeka. Alichekacheka peke yake halafu akamshukuru Mungu.
Malaika
alipomaliza kumpasha habari hiyo Anna. Akaondoka mpaka shambani alikokuwa
Joakimu amekimbilia baada ya kufukuzwa Hekaluni na Kuhani Msaidizi. Malaika
alipofika akamtokea Joakimu ambaye alikuwa na mawazo mengi kwa yale yaliyompata
kule Hekaluni. Malaika akasema Joakimu usiogope mimi niliyesimama nawe ni
Malaika Gabriel nimetumwa na Mungu kuja kukujulisha habari njema za furaha kuu
kwako na kwa mke wako. Sala zako zimekubaliwa na kupokelewa na Mungu. Na kwamba
Mke wako atapata mimba atamzaa mtoto wa kike na utampa jina la MARIA lenye
maana ya Nyota ya Bahari, Mwangaza
na Bibi. Mtoto huyu amebarikiwa kuliko wanawake wote (Luka 1:41-42) Baadae
atakapozaliwa kama mlivyoahidi ninyi wenyewe, wewe na mke wako mnapaswa
kumtolea mtoto wenu Hekaluni. Lakini Malaika alimficha Joakimu hakumwambia kama
mtoto huyo atakuwa mama wa Masiha.
Baada
ya Joakimu kusikia habari hiyo njema kutoka kwa Malaika. Naye alijawa na furaha
kubwa sana ya ajabu, hata alikaribia kufa kwa furaha hiyo aliyopata. Lakini
Mungu alimkinga kifo kisimpate. Kwa furaha hiyo mara alisahau yale yote yaliyompata
kule Hekaluni pamoja na kashifa za jirani zake. Akamtukuza Mungu kwa shangwe
moyoni mwake. Kasha Malaika akamwambia tena ili kuthibitisha habari hii njema
rudi tena hekaluni ukasali na kumtolea Mungu sadaka ileile iliyokataliwa na
Kuhani aliyekufukuza hiyo ndio shukrani kwa Mungu kwa kuwa amekuahidi kupata
mtoto. Na utakapofika huko yule Kuhani hatakufukuza tena, na pale Hekaluni
utakutana na mke wako kama ishara nyingine ya haya niliyokueleza kuwa Mungu
amenituma kwako. Baba huyo Mtakatifu kwa furaha kuu hakuchelewa alikimbia mbio
kurudi tena Hekaluni ili akathibitishe aliyoambiwa na Malaika.
Alipofika
Mlangoni mwa Hekalu kweli alikutana na Mke wake, wakakumbatiana kwa furaha kuu,
wakaingia wote Hekaluni wakamshukuru Mungu na kumtolea sadaka zao. Wakarudi
nyumbani, siku si nyingi Anna akashika ujauzito.
ANNA
ANAPAMBANA NA MISUKOSUKO YA SHETANI
Joakimu
na Anna walichaguliwa na Mungu kuwa wazazi wa Bikira Maria kwa vile walikuwa na
utakatifu wa hali ya juu sana kuliko Mwanadamu yeyote aliyewahi kuishi wakati
huo. Naye Bikira Maria alikuwa na Utukufu Mkuu na Utakatifu kupita viumbe vyote
vilivyowahi kuumbwa hapa duniani wala huko mbinguni. Mungu aliona ni vema
azaliwe na wazazi hawa Watakatifu. Furaha ya Joakimu na mkewe Anna na jamaa zao
iliendelea kuwa kubwa na mimba ya Mama Anna iliendelea kukua. Waliendelea
kumwomba Mungu mtoto azaliwe salama. Lakini palipo furaha hapakosi machukizo.
Ndipo mlaanifu Shetani na wafuasi wake walivyochukia kuona Mama huyu Mtakatifu
na jamaa zake walivyoonesha furaha yao na kusahau machungu ya matusi na
manyanyaso ya jirani zao.
Shetani
na wafuasi wake siku zote waliogopa Utabiri wa Manabii juu ya kuja kwa Masiha
ili kuikomboa dunia kutoka mikononi mwake. Ni wazi kwamba Shetani hakupenda
kabisa Mama wa Mungu azaliwe au Masiha aje duniani. Shetani alipata hofu sana
alipomwona mama huyu mcha Mungu ni mjamzito, alihisi kuwa pengine atamzaa
Masiha au Mama wa Masiha, hivyo Shetani na wafuasi wake wakapanga mbinu za
kumwangamiza Mama huyo kabla ya siku ya kuzaa kwake, ama wamuue mtoto akiwa
tumboni au mara baada ya kuzaliwa. Lakini fikra, mbinu na mipango ya shetani
kwa Mungu ni sawa sawa na ndoto za mwendawazimu. Mungu alijua mipango yote hiyo
ya shetani mapema. Mungu akamwekea Anna ulinzi wa kundi kubwa la Malaika ili
wamlinde mama na mtoto atakayezaliwa, mimba ikaendelea kukuwa na miezi ya kuzaa
kwake ikakaribia. Shetani na wafuasi wake walipojaribu kutekeleza mipango yao
wakashindwa. Ndipo walipotambua Mama analindwa na jeshi kubwa la Malaika toka
mbinguni. Hapo wakazidi kupata wasiwasi mwingi zaidi kuwa atakayezaliwa pengine
atakuwa Masiha aliyetabiriwa, au atazaliwa Mama wa Masiha. Shetani akawaambia
wafuasi wake kuwa Mama huyu ana ulinzi mkubwa sana, Hivyo kazi ya kumwangamiza
Mama ataifanya yeye mwenyewe.
SHETANI
ANAANZA MAPAMBANO
Mbinu
ya kwanza ya Shetani ilikuwa kuiangusha nyumba waliyokuwa wakiishi Joakimu na
mkewe Anna, ili iwaangukie na kuwaua wakati wakiwa wamelala usingizini. Usiku
mmoja Shetani alienda jirani na nyumba hiyo akafanya kishindo kikubwa na
tetemeko la ajabu. Akasukuma nyumba kwa nguvu zake zote; lakini alishindwa.
Malaika walinzi waliotumwa kumlinda mama na mtoto waliizuia nyumba isianguke,
hivyo mbinu ya kwanza ya shetani ikashindwa.
SHETANI
ANAJIGEUZA MSICHANA
Siku
iliyofuata Shetani alifikiria mbinu nyingine, nayo ni kujifanya binadamu.
Alijigeuza kuwa Msichana mzuri, mrembo wa kuvutia kwa sura tena mnyenyekevu
mwenye nidhamu ya hali ya juu. Akaenda kuomba kazi za nyumbani kwa Joakimu na
Anna. Kutokana na kukuwa kwa mimba Anna alihitaji msichana wa kumsaidia kazi.
Kipindi hiki alikuwa amechoka, hakuweza kufanya kazi ngumu. Kwa jinsi
alivyoonekana hakuna mtu aliyeweza kumtambua kuwa alikuwa shetani, watu wote
walimwona sawa na watu wengine. Hata Joakimu na Anna hawakumtambua alipofika
kuomba kazi. Shetani alipofika akawasalimu na kujieleza kuwa anaomba kazi za
ndani. Yeye ni msichana ambaye bado hajaolewa. Tena ni fukara na wazazi wake
walifariki siku nyingi. Hana chakula wala mahali pa kuishi, anatangatanga na
maisha ni ya taabu sana, kwa maelezo hayo Joakimu na Mke wake wakamwonea
huruma, wakamwajiri.
Anna
alifurahi kupata msichana wa kumsaidia kazi za nyumbani katika kipindi hicho
cha ujauzito. Msichana Shetani akakaribishwa na kupatiwa chumba cha kulala na
siku iliyofuata akaanza kazi. Siku za mwanzo alionesha tabia ya upole,
unyenyekevu, heshima na tena mchapa kazi hodari. Mzee Joakimu na Mkewe
wakampenda sana msichana huyu. Lakini Shetani ni shetani tu. Kadri alivyozidi
kuishi pale nyumbani tabia yake ilianza kubadilika, akaanza kuwa kiburi na
matusi yenye kashifa kama zilizokuwa zinafanywa na jirani zake Joakimu na Anna.
Lakini familia hii Takatifu bila kujua walimkaribisha shetani, waliendelea
kumpenda na kumuombea kwa Mungu ilia ache tabia hizo mbaya.
Basi
siku moja Msichana shetani alipanga kutimiza mpango wake wa kumwangamiza Mama
na Mtoto. Akaazimia kumwekea sumu Anna katika chakula au kinywaji. Mungu
akamwonea huruma Anna. Akawaamuru wale malaika walinzi kumfukuza Msichana
Shetani. Malaika wakamfukuza. Joakimu na Anna walishangaa kuona msichana wao wa
kazi ametoweka ghafla bila kuaga. Ndipo
walipogundua kuwa hakuwa binadamu wa kawaida bali walikuwa wamemkaribisha
shetani. Hata hivyo Shetani hakuchoka kuja mara kwa mara kujaribu mbinu mpya za
kumwangamiza Mama na mtoto tumboni, lakini alishindwa kwa kuwa Malaika walinzi waliimarisha ulinzi
mkali siku zote.
BIKIRA
MARIA ANAZALIWA
Hata
siku ya kumzaa Bikira Maria ilipofika, Mungu alimjulisha Anna katika mawazo
kuwa muda wa kujifungua mtoto umefika. Kwa vile alikuwa ameomba kwa Mungu
kwamba Mtoto anapozaliwa asishikwe na mtu yeyote. Ili kuonesha ombi lake
lilikuwa limekubaliwa na Mungu, muda wa kujifungua mtoto ulipofika, Mume wake
alipewa usingizi mzito asiweze kumwona mtoto wakati wa kuzaliwa kuzaliwa kwake.
Japo walikuwa pamoja chumbani. Tena Mungu alimkinga Mama asipate uchungu wa
kuzaa kama desturi. Mtoto alipozaliwa alipokelewa na Malaika.
Mungu
kwa kupitia Malaika, Anna alijulishwa kuwa mtoto aliyezaliwa anapaswa kulelewa
kama watoto wengine. Lakini apewe heshima ya pekee kwa kuwa atakuwa mama wa
Mungu. Heshima hiyo aiweke moyoni mwake wala asioneshe kwa watu wengine,
Malaika Makundi kwa makundi walishuka kutoka mbinguni. Hesabu yao haijulikani.
Wakajumuika na wale Malaika walinzi. Huku wakiimba nyimbo nzuri na kumsifu
Mungu. Zilikuwa nyimbo nzuri za kumsifu Mungu, zilikuwa nyimbo za kuvutia sana.
Anna alijaliwa kuwaona Malaika na kuyaona mambo yote wazi wazi kwa macho yake
yaliyofanyika na kusikia nyimbo za Malaika. Kwa furaha kuu akamshukuru Mungu
kwa kumpata mtoto.
Baada
ya kujifungua ndipo alipomwamsha Mume wake. Joakimu alishangaa kuona Mke wake
amepata mtoto bila mkunga yeyote wa kumsaidia. Kwa furaha alipiga magoti na
akasujudu. Wote kwa pamoja wakasali, wakamshukuru Mungu, wakiwa na furaha ya
ajabu isiyoelezeka. Furaha ilikuwa kubwa sana kupita hata ile ya kwanza
walipopashwa habari na Malaika juu ya kupata mtoto. Hakika ilikuwa shangwe kuu.
Joakimu akamchukua mtoto mikononi mwake akamtolea kwa Mungu ili kutimiza ahadi
yao. Mtoto alizaliwa saa 6:00 usiku, tarehe 8 September. Hivyo ndivyo
alivyozaliwa Mtoto Maria Mtakatifu na maajabu yake. Kanisa Katoliki huadhimisha
sikukuu ya kuzaliwa Bikira Maria tarehe 8 September ya kila mwaka.
Kesho
yake asubuhi watu wengi walifika nyumbani pale. Kumsalimu mtoto na kuwapongeza
wazazi hawa. Watu wote waliofika walikuwa na furaha kubwa. Walileta mikononi
mwao zawadi nyingi za aina mbalimbali zenye kuvutia. Siku ya nane wazazi hawa
walimpa jina mtoto wao akaitwa Maria. Siku hiyo Joakimu alitayarisha sherehe
kubwa sana. Watu wengi walihudhuria wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki. Pia
walikuwepo wale jirani zao waliokuwa zamani wakiwatolea kashifa na matusi. Malaika
wa Mungu nao walihudhuria. Walikuwa wengi sana. Waliimba nyimbo zao nzuri za
kumsifu Mungu. Anna peke yake aliendelea kuwaona na kusikia nyimbo hizo za
Malaika. Lakini Mume wake na watu wengi wengine hawakujaliwa bahati ya kuwaona
wala kusikia nyimbo zao. Siku hiyo ilikuwa ya furaha kubwa mno. Watu walikula
na kunywa hata kusaza. Walimshukuru na kumtukuza Mungu mkuu. Wakiwaombea Baraka
za Mungu, wazazi hawa na mtoto wao. Tangu siku hiyo wazazi hawa walianza
kuheshimiwa na kuthaminiwa kama watu wengine wenye watoto katika kabila lao.
Joakimu
na Anna wakaishi sasa kwa Amani na furaha kubwa katika ile jamii
iliyowazunguka. Wakamlea mtoto wao katika kweli na haki. Huku wakiomba Masiha
aje haraka.
MAISHA
YA BIKIRA MARIA AKIWA MTOTO
Bikira
Maria akiwa Mtoto alikuwa mchangamfu sana. Alipenda ukimya, hakupenda kulialia
au kudeka kama walivyo watoto wengine kwa wazazi wao. Kwa tabia hiyo watu wengi
walimpenda sana, hata yeye mwenyewe aliwapenda sana watu wote waliofika
nyumbani kwao na kumpakata. Jambo lililowashangaza wazazi wake na watu wengine
mtoto huyu wakati alikuwa bado hajaweza kukaa chini peke yake wala kusema;
lakini alionekana ana hekima kama mtu mzima, alikuwa anaelewa kila kitu
kinachosemwa au kutendwa. Mtoto Maria alikuwa ana ulimi mzito hakuweza kuongea
mapema, mpaka alipotimiza umri wa Mwaka mmoja na miezi sita ndipo alipoanza
kuongea. Wazazi wake na watu wengine walidhani pengine angekuwa bubu.
Alipotimiza
umri wa miaka miwili, Mama yake alianza kumfundisha kusoma na kazi nyepesi.
Aliongozana
naye kwenda kutoa misaada kwa masikini. Tabia hii mtoto Maria ilimfurahisha
sana, aliipenda na kuizoe haraka. Kila mara walipofika pale kwa masikini Mama
yake alimzoesha kumpa Mtoto zawadi walizokuwa wamekuja nazo ili awagawie
masikini. Halafu alimfundisha baada ya kuwagawia zawadi, kuwabusu wale masikini
mikono na miguu yao. Kuna wakati Fulani Mtoto aliwagawia masikini nusu ya
chakula chake alichopewa siku hiyo kula yeye mwenyewe jambo ili pia
liliwastaajabisha sana wazazi wake. Siku zilipozidi mtoto alizoea kazi hii.
Mwisho alikuwa anakwenda peke yake kuwahudumia wale masikini.
Zipo
siku alizokwenda kuwapelekea zawadi wale masikini akawakosa. Mtoto alisikitika
sana moyoni kuwakosa rafiki zake wapenzi, kwa heshima ya rafiki zake hawo
aliamua kubusu ardhi eneo walilopendelea kukaa ama kupita wale masikini.
BIKIRA
MARIA NA WAZAZI WAKE WANAONA MAONO
Mtoto
Maria akiwa na wazazi wake nyumbani kwao Nazareti, kwa pamoja walikuwa wameketi
sebreni. Ghafla waliona maono ya Utatu Mtakatifu ambao ulimwambia mtoto huyu
Mtakatifu kuwa inampasa kujitolea mwenyewe kwa Mungu ili awe Mtumishi wa
Hekaluni. Pia Utatu Mtakatifu uliwakumbusha wazazi wake kuwa siku zimekaribia
za kumtolea mtoto wao kwa Mungu Hekaluni kama walivyoahidi kabla ya kuzaliwa
mtoto huyu. Mama yake Maria aliposikia
habari hiyo alijisikia uchungu mkubwa wakutengana na binti yao waliomzoea na
kuwachangamsha. Mungu aliuona uchungu wa Mama huyu akamuonea huruma akampoza
machungu yake.
BIKIRA
MARIA ANATOLEWA KWA MUNGU HEKALUNI
Siku
zilienda mbio, mtoto alipotimiza umri wa miaka mitatu. Wazazi hawa Watakatifu
walipanga safari ya kumpeleka mtoto wao hekaluni, ili kumtolea kwa Mungu kama
walivyohaidi. Siku ilipofika Mama alimbeba mtoto akiongozana na Mume wake.
Safari hiyo ilikuwa ndefu walitoka Nazareti kwenda Yerusalemu umbali wa maili
68 kwa kutembea kwa miguu lakini ilikuwa safari ya furaha kwa wazazi hawa na
mtoto wao. Kundi kubwa la Malaika wa Mungu liliwasindikiza, Mtoto Maria
aliwaona Malaika hao. Ila wazazi wake walifumbwa macho na Mungu hawakuweza kuwaona
Malaika.
Walifika
salama Yerusalemu, katika viwanja vya Hekalu, Mama akamtelemsha Mtoto. Kwa
mapendo makubwa wazazi wote wawili wakamshika mikono mtoto wao, mmoja kulia na
mwingine kushoto. Mtoto akawa katikati ya Baba na Mama yake wakatembea polepole
kuelekea jingo la Hekalu kuu, walipofika lango kuu wakaingia ndani pamoja,
wakapiga magoti, humo hekaluni walimkuta kuhani Mkuu akisali. Joakimu na Anna
wakasali sala ya kumtolea mtoto kwa Mungu na Mtoto Maria akasali sala
yakujitolea yeye mwenyewe kwa Mungu. Baada ya sala zao kukasikika sauti ya
upole ndani ya jengo lote la hekalu iliyosema.
"KARIBU
MCHUMBA WANGU MPENZI, KARIBU HEKALUNI MAHALI AMBAPO NAPENDA KUSIKIA SAUTI YAKO
NZURI YA KUNISIFU". Sauti waliisikia watu wote waliokuwemo Hekaluni. Baada
ya sala wazazi na mtoto waliinuka walipokuwa wamepiga magoti wakamuongoza mtoto
mahali alipokuwa ameketi Kuhani Mkuu Simoni wakamkabidhi mtoto wao.
Kuhani
Mkuu akampokea mtoto. Halafu akawaongoza wazazi na mtoto mpaka kwenye nyumba ya
malezi, walipokuwa wanalelewa Mabinti wote wa ukoo wa Yuda na Lawi mpaka
walipofikia umri wa kuolewa ndipo waliruhusiwa kurudi makwao au waliopenda
walibaki pale kwa maisha ya kitawa, nje ya jengo hilo walimkuta Kuhani mdogo
amesimama kwenye ngazi za kwendea langoni, jengo hilo lilikuwa na ngazi kumi na
tano za kupanda kabla ya kufikia mlango wa kuingia. Kuhani mdogo akawapokea
akambeba mtoto ili kumpandisha kwenye ngazi, alihofia akipanda peke yake
pengine angeweza kudondoka chini kwasababu ya ulefu wa ngazi hizo.
Kutokana
na sheria za nyumba ya Malezi, haikuruhusiwa kuingia ndani ya nyumba ya malezi
mtu yeyote asiyekuwa mtumishi au mlezi wa mabinti hao. Hivyo kuhani mdogo
alimsimamisha mtoto kwenye ngazi ya kwanza ili awaage wazazi wake. Mtoto Maria
alipiga magoti kuwaelekea wazazi wake. Halafu akaomba Baraka zao, wazazi wake
wakambariki naye akabusu mikono yao.
Baada
ya kupata Baraka, mtoto Maria bila yakujali au kuonesha uchungu wakutengana na
wazazi wake tena bila kusubiri kuongozwa au kubebwa tena kuhani mdogo; yeye
mwenyewe kwa haraka aliparamia zile ngazi mpaka akaufikia ule mlango wa
kuingilia. Akapiga hodi na kuingia ndani, wakati huo wazazi wake pamoja na
Makuhani walikuwa bado wapo pale nje, walishangazwa kuona ujasiri wa Binti
huyu.
Makuhani
wakasema hawajawahi kuona ujasiri mkuu wa namna hiyo kati ya Mabinti wote
waliowai kupokelewa pale baada ya maongezi hayo, Joakimu na Anna wakaagana na
Makuhani wakarudi nyumbani kwao kwa furaha.
BIKIRA
MARIA KATIKA NYUMBA YA MALEZI
Mtoto
Maria baada ya kufunguliwa mlango na kuingia katika nyumba ya Malezi, Mabinti
wenzake waliokuwa wanalelewa humo pamoja na Mama walezi walimpokea kwa furaha
na mapendo makubwa. Kuhani Mkuu Simoni alimteua Mama mmoja awe mlezi wa mtoto
huyu ambaye alijulikana kwa jina la Anna jina la Mama huyu lilifanana na jina
la Mama mzazi wa Maria. Mama huyu alikuwa na sifa ya kutabiri mambo yajayo.
Mama huyu alikubali kuwa mlezi wa mtoto huyu kama alivyoteuliwa na Kuhani Mkuu.
Mtoto
Maria alipotambulishwa kwa Mama mlezi wake alifurahi sana, akachukua vitu
alivyotoka navyo nyumbani, zikiwemo pesa na nguo zake akamkabithi mlezi wake
ili awagawie masikini. Yeye alibaki na vitu vichache tu, na nguo alizokuwa
amevaa. Basi jambo hili liliwastajaabisha Sana wenzake pamoja na walezi wao.
Kwa hali hiyo akaonekana Binti masikini kuliko wote. Hata baadhi ya mabinti
wenzake walivyoona hivyo palepale wakaanza kumdharau mioyoni mwao.
Usiku
ulipoingia bila mtu yeyote kujua, mtoto Maria alichukuliwa na Malaika mpaka mbinguni
mbele ya Utatu Mtakatifu. Alipofika huko akaahidi kuwa atakuwa mtawa maisha
yake yotekatika nyumba ya malezi.
Siku
iliyofuata mama mlezi wake alianza kazi yake ya kwanza ya kumfundisha sheria za
kitawa .nazo zilikuwa tatu .kwanza utii, pili umasikini na tatu usafi wa roho
na mwili.baada ya siku chache kuhani mkuu akamwapisha .naye akaweka nadhiri ya
kuishi kitawa kwa maisha yake yote mpaka kufa.
TABIA
YA MTOTO MARIA KATIKA NYUMBA YA MALEZI.
Maisha
ya utawala ya mtoto huyu katika nyumba ya malezi yalianza vizuri bila matatizo
yoyote.mama mlezi wake alimuongoza vizuri, alipenda maandiko matakatifu kwa
kujisomea na kufanya kazi nyingine kadiri alivyoelekezwa.
MARIA
ANALETEWA TAARIFA YA KIFO CHA BABA YAKE
Baada
ya miezi sita kupita, Mungu aliwatuma Malaika wamjulishe kuwa Baba yake mzazi
atakufa muda mfupi ujao. Mtoto alimshukuru Mungu kwa kumpelekea habari hiyo.
Taarifa haikumtia hofu wala masikitiko kwakuwa alijua kila mwisho wa maisha ya
binadamu ni kifo.
Akamuomba
Mungu kupitia wale Malaika amjalie Baba yake afe kifo chema, walezi wa Maria
nao walipelekewa taarifa ya kifo cha Mzee Joakimu, lakini Maria hawakumruhusu
kwenda kumzika Baba yake kwa vile walitaka kuona kama anaiweza ile amri ya
kitawa ya kuwa mtii kwa viongozi wake.
Maria
alikuwa akilindwa siku zote na Malaika kumi na wawili. Na alikuwa akiwaona
akawaruhusu hao Malaika walinzi wake waende kumlinda Baba yake na Mashambulio
ya shetani saa ya kufa.
Mungu
alifurahishwa sana na maombi ya Maria
pia kuwaruhusu wale Malaika walinzi wake waende kumlinda Baba yake, Mungu
akatuma jeshi kubwa la Malaika nao wakajumuika na wale Malaika walinzi wakaenda
kumlinda mzee huyu Mtakatifu. Malaika walipofika kwa mzee Joakimu, Mungu
akamfunulia macho akawaona hao Malaika kwa macho yake. Nao Malaika wakamjulisha
kuwa wametumwa na Binti yake kwa ruhusa ya Mungu waje kumlinda dhidi ya
mashambulio ya shetani katika saa yake ya mwisho. Mzee alifurahi sana
akamshukuru Mungu na mwanaye kwa fadhila hiyo kuu. Maria alijua pia kuwa Mungu
amewatuma idadi kubwa ya maelfu ya Malaika ya kumlinda Baba yake. Naye
alifurahi sana na kumshukuru Mungu.
Mzee
Joakimu dakika chache kabla ya kufa alifunuliwa na Mungu ile siri aliyoambiwa
Mke wake siku aliyozaliwa mtoto wao, kuwa "Mtoto wao alikuwa Mama wa
Masiha aliyetabiriwa na manabii, na kwamba amebarikiwa kuliko wanawake wote na
Ukuu wake ni wa pili kutoka kwa Mungu." Mzee alifurahi sana moyoni mwake
akatabasamu, akamshukuru Mungu, halafu akakata roho akiwa amelala kitandani.
Mke wake akiwa karibu naye amesimama upande wa kichwani mwa kitanda. Alikufa
kifo kitakatifu chenye furaha yakumuona Mungu. Baada ya kifo cha mzee huyu, Mke
wake alitoka akawajulisha majirani zao. Ndugu na jamaa walifika wakamlilia Baba
huyu Mtakatifu. Mwili wake ukazikwa kama ilivyo desturi na mila zao. Roho yake
ikachukuliwa na malaika ikapelekwa limboni.
BIKIRA
MARIA ANAJARIBIWA NA SHETANI
Shetani
aliona Mzee Joakimu analindwa na kundi kubwa la Malaika kabla ya kufa na hata
wakati wa mazishi yake, kwasababu hiyo hakuweza kumshambulia hata kidogo.
Akakasirika sana, hivyo akamuomba Mungu ruhusa aende nyumba ya Malezi
akamshambulie mtoto Maria ili amtukane Mungu apate kufukuzwa Utawani. Mungu
alikubali akamruhusu Shetani akaenda katika nyumba ya malezi, alipofika huko
jaribio la kwanza lilikuwa kumfumba macho asiweze kuwaona wale malaika wa Mungu
waliokuwa wakimlinda, wala hakuweza kusema nao hali hiyo ilimshtua sana, ikampa
uchungu moyoni. Tena akajisikia mpweke alifikiri na kujihoji akilini kwanini
hali hii imetokea hivi? Akawaza kuwa pengine amemkosea Mungu kwa namna flani
ndio maana macho yake yamefumbwa asiwaone tena Malaika na kuongea nao.
Siku
zilizivyozidi akafumbwa zaidi hata hakuweza kumuona Mungu tena kama zamani,
hali hiyo ilimzidishia uchungu na mawazo mengi moyoni.
Bikira
Maria hakujua hizo zilikuwa mbinu za shetani, akahuzunika sana moyoni.
Akaanza
kumuomba Mungu wale Malaika wamjulishe kama kuna jambo amekosea ili amuombe
toba. Akasali akasema "Mungu wangu mimi najiona mdogo kuliko viumbe vyote
vilivyoko mbinguni na duniani. Japo umeniachia vinitulize lakini mimi
sivitamani hata kidogo natamani tu Mungu wangu kukuona wewe Mchumba wangu".
Katika
nyumba ya malezi alipedwa sana na Makuhani, Mama walezi na mabinti wenzake
kwasababu ya unyenyekevu, upole na heshima yake kwa watu wote. Ingawa baadhi ya
wasichana wenzake walimdharau kwa vile alikuwa amebaki fukara bila nguo na vitu
vya thamani baada ya kugawa vitu na nguo zake kwa masikini.
Jaribio
la pili, Shetani aligundua kuwa Bikira Maria alikuwa anapendwa na watu wote.
Akatafuta mbinu nyingine ili achanganyikiwe zaidi na halafu amtukane Mungu,
Shetani na wafuasi wake wakawaingia wale wasichana wengine waliokuwa
wakielewana naye. Mioyo yao ilijaa husuda wakaanza kumchukia sana na kumtukana
wakisema; Maria mnafiki mpenda kujipendekeza kwa wakubwa tena mchongezi mkubwa.
Lakini yeye alipotukanwa hakuwajibu neno lolote alinyamaza tu.
Wasichana
hao walipoona hajibu neno lolote walianza kumchongea kwa wakubwa wao, Maneno ya
uwongo ili afukuzwe napo wakashindwa.
Siku
nyingine wasichana hao wakamchukua wakamuingiza katika chumba kimoja wapo
kilichotumika kwa maongezi, kilikuwa chumba safi na chenye utulivu usioweza
kupenyeza kelele yeyote ile, walipofika humo walianza kumtukana sana halfu
wakampiga makofi, kelele zikawa nyingi mwisho mama walezi wakasikia wakaja
mbio. Walipofungua mlango wa chumba hicho wakawakuta wale wasichana wamemvamia
Maria wakimshambulia kwa maneno na kumpiga.
Wale
wasichana walipoona wamegundulika na wakubwa wao, wakaanza kujitetea wakisema.
Wapendwa Mama walezi wetu, Msichana huyu ni mtu mbaya sana. Tulikuwa
kutiwaambia hamkumchulia hatua yeyote. Tazameni siku zote akiwa mbele yenu
hujifanya mtu safi lakini tukiwa naye ni mtu mwenye matusi na fujo nyingi,
hivyo leo tupo hapa ilikumfundisha adabu njema, tena mara nyingi tukimshauri
yeye huwa hataki kutusikiliza au kufuata ushauri wetu pia wakati mwingine huwa
anatupigia magoti ya kutuziaki akiomba tumsamehe halafu amekuwa mtu asiyetaka
kubadili tabia yake. Uwongo huo wa wasichana hawa baada ya mama walezi kuhusikiliza
kwa makini ukakubalika. Kwa vile yeye hakuweza kujitetea kutokana na kipigo
alichopata kutoka kwa wenzake na kuendelea kumzomea. Shauri hili likawafikia
Makuhani akapewa karipio kali na akatakiwa ajirekebisho vinginevyo atafukuzwa
utawani.
Shetani
alipoona hayo alifurahi sana, akazidisha mapambano vita hii ya shetani na
Bikira Maria ilidumu kwa kipindi cha miaka saba kila siku kulitokea hili ama
lile lililomhusu na kumuudhi au kumkosesha raha, siku nyingine tena wale
wasichana wenzake walimshitaki tena kwa walezi wao walimsingizia kuwa Maria
bado anaendelea na matusi na ukorofi wake hivyo akapendekezwa afukuzwe utawani.
Makuhani wadogo na walezi waliposikia malalamiko hayo wakafanya mkutano
kujadiri wafanye nini. Mwisho wa mkutano wao huo wote wakakubaliana kuwa
Afukuzwe na arudishwe nyumbani kwao.
Katika
kipindi chote alichokuwa akisingiziwa na kupigwa na wenzake, Maria siku zote
alikuwa akimuomba Mungu ayaone mateso yake na amuhurumie pia aliwaombea sana
adui zake na wakuu wake waweze kugundua fitina za adui zake. Maamuzi ya hao
Makuhani na walezi ya kumfukuza utawani binti huyu yalipelekwa kwa Kuhani Mkuu
Simon ili yapate Baraka zake. Kuhani Mkuu alipoyapokea akayabatirisha maamuzi
haya akapendekeza apewe tena karipio kali sana. Binti huyu akaitwa na walezi
wake akaonywa vikali sana.
Masikini
Binti huyu alitoka kwa walezi wake akilia machozi kwa ajili ya maneno
aliyoambiwa na walezi wake, kwani yalikuwa makali sana. Alipotoka nje wale adui
zake walipomuona anakuja akilia walifurahi sana hata shetani alifurahi pia, ila
hawakufurahi kuona hakufukuzwa utawani kwasababu hiyo wakapanga mbinu nyingine
mpya na kubwa zaidi kuliko zote walizowai kuzifanya.
Chuki
ikazidi sana kati yake na wale wasichana wenzake. Shetani akawapa mawazo mapya
wakapagawa sana. Wakaitana na kufanya mazungumzo yao ya faragha bila
kumshirikisha. Katika mazungumzo yao wakaadhimia wafanye mambo mawili. Kwanza
kumfanyia mambo machafu ili kuharibu ubikira wake ili apatikane sababu ya
kufukuzwa utawani. Pili au wamuuwe kwa kutumia njia yoyote watakayoweza na
ambayo haitagunduliwa kwa makuhani na mama walezi.
MUNGU
ANAINGILIA KATI
Mungu
alipotambua nia mbaya za maadui wa Binti huyu akaingilia kati ili kumlinda
Mtumishi wake mwaminifu. Usiku Mungu akawaotesha ndoto Mama Mlezi na Kuhani
Mkuu Mungu akazungumza nao usingizini akasema. Maria ni Mtumishi wangu
mwaminifu anayependeza machoni pangu kwa vile ni mwaminifu daima mashitaka
yanayotolewa juu yake kwenu na wasichana wenzake yote sio ya kweli hata kidogo.
Hata ilipofika asubuhi Kuhani mkuu na Mama mlezi wa Maria wakakutana na
kusimuliana ndoto hiyo kila mmoja alivyoota. Wakagundua kuwa Mungu amesema nao
usingizini. Wakaamua kumuita Binti huyu Mtakatifu na kumuomba msamaha kwa jinsi
ya awali walivyomkaripia vikali. Naye akasema kwa unyenyekevu "Nasitahili
maonyo yoyote kwa makosa yangu niliyofanya na nitakayofanya, tena nipo tayari
kutii chochote mtakacho niamuru".
KIFO
CHA ANNA MAMA MZAZI WA BIKIRA MARIA
Maria
Bikira Mtakatifu alipotimiza umri wa miaka kumi na miwili (12) aliletewa
taarifa na Malaika kuwa Mama yake Mzazi karibu atakufa. Binti huyu hakuweza
kuwaona Malaika kwa macho walipomletea habari hii ya kifo cha Mama yake, kwani
alikuwa bado amefumbwa ila taarifa hiyo aliipokea kwa kusikia sauti tu. Baada
ya kupata taarifa hiyo alipiga magoti akamuomba Mungu akasema "Mungu wangu
nakuomba umjalie Mama yangu afe kifo chema, kwani wewe wajua kuwa alikuwa
mtumishi wako mwaminifu". Basi baada ya sala hiyo Mungu hakumjibu kwa
maneno ila aliwaamuru wale Malaika waliokuwa wakimlinda wamchukue msichana huyu
mpaka nyumbani kwao Nazareti akaonane na Mama yake kabla ya kufa. Wale Malaika
wakamchukua bila ya mtu yeyote kujua wakampleka kama walivyoamuriwa na Mungu.
Malaika
walipomfikisha nyumbani kwao akaonana na Mama yake, Mama yake alifurahi sana
kuonana na Binti ye kwa mara ya mwisho. Maria pia alifurahi kuonana na Mama
yake baada ya kutengana naye kwa muda wa miaka 9. Mtoto na Mama yake wakaagana.
Maria akaomba Baraka ya mama yake, Mama akambariki Binti ye baada ya Baraka
Mama huyu Mtakatifu akiwa na sura ya furaha akamuomba bintiye amfumbe macho
baada ya kufa kwake. Muda mfupi Anna akiwa amelala kitandani kwake akakata roho.
Akafa
kifo chema na kitakatifu, Mtoto akamfumba macho Mama yake kama alivyokuwa
ameelekezwa. kule utawani alibaki Malaika Mmoja ambaye amejigeuza sura
akaonekana kwa viongozi wa utawani na kwa watawa wengine kama Bikira Maria.
Hivyo hawakuweza kugundua kama binti huyu Mtakatifu hayupo pale na kwamba
amepelekwa Nazareti kuagana na mama yake.
MAZISHI
YA MAMA YAKE
Jirani
zake walipopata habari ya kifo cha mama huyu walikusanyika na wakautayarisha
mwili wa mama huyu kama ilivyo desturi na kufanya mipango ya mazishi. Watu
wengi walihudhuria msiba huu. Wakati watu walipouchukua mwili kwenda kuuzika,
Malaika nao wakamchukua Bikira Maria na kumrudisha utawani. Akaendelea na
shughuli za pale utawani kama kawaida huku akimshukuru Mungu kwa kuwatuma
Malaika wampeleke kuagana na Mama yake na kushuhudia kifo chake. Lakini moyoni
na akilini akawa na hisia kuwa wakati wa kuweza kumwona Mungu tena na wale
Malaika uso kwa uso umekaribia. Akapiga magoti akasema. Malaika wangu wapenzi
naomba mnijulishe lini nitawaona tena na kumwona Mungu kwa macho yangu. Nao
Malaika wakamjibu wakasema; - utatuona hivi karibuni, muda wa kutuona na
kumwona Mungu umekaribia mara baada ya maneno hayo ya Malaika; macho yake
yakafumbuliwa, akauona Utatu Mtakatifu na wale Malaika kama mwanzo. Akafurahi sana,
akamshukuru Mungu.
BIKIRA
MARIA ANATOKEWA NA ROHO MTAKATIFU.
Mwaka
mmoja na miezi sita baada ya kifo cha Mama yake wakati huo akiwa na umri wa
miaka kumi na mitatu na miezi sita. Alitokewa na Roho Mtakatifu aliyetumwa na
Mungu ambaye alimfahamisha kuwa kutokana na mapenzi ya Mungu, licha ya kuwa
yeye ni Mtawa; lakini atapata mchumba na ataolewa. Tena mtoto atakayempata
amtolee Hekaluni kama vile Nabii Ibrahimu alivyomtolea Mwanae Isaack kwa Mungu
awe sadaka ya kuteketezwa. Msichana huyu alishangaa sana kupata ujumbe huu.
Kasha akajisemea moyoni, itakuwaje jambo hili? Mbona mimi ni Mtawa na mtumishi
wake Mungu Hekaluni! Alijisemea hayo
moyoni kwa sababu alikumbuka tangu alipokuwa na umri wa miaka mitatu alipoingia
kwenye nyumba ya malezi, alijitolea kuishi kitawa mpaka kufa. Baada ya
kutafakari hayo mara akajibu akasema. Bwana anitendee anavyotaka. Mungu
akaahidi kumlinda na kila hila za Shetani na kwamba atakuwa nae siku zote. Kwa unyenyekevu
mkubwa na upole, huku akiwa na hofu kubwa kwa mambo yajayo, akasubiri Mungu
atakavyomtendea.
KUHANI
MKUU NA MAMA MLEZI WANAOTA NDOTO.
Mji
wa Yerusalemu wakati huo ulikuwa na mzee mmoja jina lake aliitwa Simoni, huyu
ndiye yule Kuhani mkuu mwenye sifa kubwa ya kumcha Mungu, siku moja alitokewa
na Roho Mtakatifu katika usingizi, akaota ndoto ya ajabu, ndoto hiyo ilimtaka
afanye matayarisho ya kuolewa kwa Bikira Maria Mtawa. Binti wa Joakimu na Anna.
Binti aliye mtumishi wa Bwana. Mwaminifu kwa Mungu na watu wote. Ndiyo ilikuwa
sifa yake kwa wale watu waliopata kumfahamu wakati ule.
Kuhani
Mkuu alipoamka akaikumbuka ndoto yake. Akashangazwa mno na ndoto hiyo kwa
sababu alimjua binti huyu kuwa ni Mtawa. Lakini ghafla akiwa bado amezama na
mawazo akilini na rohoni mwake kuhusu ndoto ile, Roho Mtakatifu akamtokea
waziwazi. Akamwambia asiwe na wasiwasi wala asishangae kwani hayo ndiyo
yalikuwa matayarisho ya kuja kwa Masiha aliyetabiriwa na Manabii. Basi Kuhani
mkuu akiongozwa na huyo Roho Mtakatifu, akawaita Makuhani wote wa chini yake,
wasomi mbalimbali pamoja na wavulana wote ambao wakati huo walikuwa bado
hawajaoa, akawaeleza jinsi Mungu alivyomwongoza atangaze juu ya kumpata mtu
atakayekuwa mume wa Bikira Maria Mtawa. Vijana walifurahi sana kusikia habari
hii. Kwakuwa walikwisha sikia sifa nzuri za Msichana huyu. Kila mmoja alitamani
awe Mume wa Binti huyu. Na katika vijana wote, alikuwepo kijana mmoja aliyekuwa
naye amejitolea tangu utoto wake aishi maisha ya bila ndoa. (Maisha ya useja)
kweli kijana huyu habari hii haikumfarisha hata kidogo, ndiye Yoseph
(Mseremala) miezi sita ilipita baada ya vijana na Makuhani kupewa taarifa hiyo.
Ndipo kuhani Mkuu alipowaita tena Hekaluni ili kufanya maombi na mafungo ili
Mungu awaoneshe ni nani atakayekuwa mume wa Bikira Maria Mtawa. Wavulana wote
wenye umri wa kuoa walifika. Humo Hekaluni Kuhani Mkuu aligawa fimbo kavu kwa
kila kijana aliyehudhuria.
Naye
Yoseph Mseremala alikuwepo, Kuhani Mkuu baada ya kuwagawia fimbo hizo
akawafahamisha vijana hao kuwa fimbo itakayochipua ua jeupe, itakuwa
utambulisho wa Mungu kuwa mwenye fimbo hiyo ndiye atakuwa Mume wa Bikira Maria
Mtawa. Mfungo wa maombi yakaanza. Mafungo yalikuwa ya siku tisa. Katika maombi
hayo Yoseph yeye aliomba Mungu amwepushe na hilo. Na kwamba amjalie neema ya
kuishi kitawa mpaka kufa, akitunza usafi wa mwili na roho yake. Lakini mambo
yakamgeukia, fimbo yake Yoseph pekee ilionekana imechipua ua jeupe. Ishara
nyingine ilimtokea, njiwa mweupe alitua kichwani pake. Makuhani na wale
wavulana wenzake waliokuwepo nae wakashuhudia, ikajulikana Yoseph amechaguliwa
na Mungu kumwoa Bikira Maria mtawa. Akiwa ameshikwa na butwaa kuona fimbo yake
ndiyo iliyochipua ua akatamani kukimbia mbio; akashindwa. Kuhani Mkuu
akamtangaza rasim kuwa ndiye mteule wa Bwana atakayefunga ndoa na Maria mtawa.
Wote waliokuwepo hekaluni wakamshangilia kwa vifijo na nderemo. Vijana wenzake
wakampa mkono wa pongezi. Kati yao vijana wengine baada ya kuona hivyo
waliondoka kwa shingo upande kwa kuwa hawakupata bahati ya kuchaguliwa,
Makuhani nao walimpongeza sana Yoseph.
Kuhani Mkuu Simoni na Mama Mlezi Anna wakampa mkono wa pongezi Bikira Maria kwa kuonesha tabia nzuri katika maisha ya kitawa walimuomba msamaha kwa jinsi awali uongozi walivyokuwa wanampa hukumu ya makaripio na mashitaka ya uwongo yaliyosemwa na wasichana wenzake katika nyumba ya malezi ya utawa.
NDOA
INAFUNGWA
Kuhani
Mkuu akaagiza Maria mtawa aletwe ili ndoa ifungwe, binti akaletwa huku
akionekana anang´ara kwa utukufu wa Mungu kama Malaika alipofikishwa
hekaluni ndoa ikafungishwa na Kuhani Mkuu. Vifijo na nderemo vilisikika kutoka
humo kwa watu wote waliohudhuria sherehe hiyo, watawa wenzake Maria
wakampongeza na kumuaga, Makuhani na Mama walezi nao wakawapongeza wanaharusi
hawa na kuwaaga, kwa kutoa Baraka zao. Siku watakatifu hawa walipofunga ndoa
yao. Maria Bikira Mtakatifu alikuwa ametimiza umri wa miaka kumi na mine (14)
kamili.
BAADA
YA NDOA
Baada
ya ndoa ya kufungwa Yoseph na Maria walikwenda kuishi kwa muda Yerusalemu
kwenye nyumba yao ya chumba kimoja. Iliyokuwa imejengwa kwa mawe ndio nyumba
aliyojenga na kuishi Yoseph kisha walihamia Nazareti katika nyumba waliokuwa
wanaishi Joakimu na Anna. Bikira Maria ndiye aliyemshauri Mme wake kuhamia huko
alifanya hivyo ili akarisishwe mali zote zilizoachwa na wazazi wake baada ya
kufariki. Walipofika huko Maria alipewa urithi wa mali zote, naye akachukua
sehemu ya mali hizo zingine akazigawa kwa ndugu zake, kwa masikini na kwa Mume
wake.
MAISHA
YA NDOA YAO
Kwa
desturi ya mila zao Mvulana na Msichana wakifunga ndoa huwa mwiko kabisa
kushiriki tendo la ndoa (Kujamiana), ingawa huruhusiwa nyumba moja desturi hii
udumu kwa muda flani kadri ya maamuzi ya wazee wanaolinda sheria na mila
wanavyoona inafaa na kuwapangia kipindi hiki huwaangaliwa kama wakati wa
uchumba na kufahamiana tabia. Nao watakatifu hawa walizifahamu sheria na Mila
zao, waliziheshimu na kuzifuata walielewa kwamba wakizikiuka watapaswa
kushitakiwa kwa Kuhani na adhabu yake ilikuwa kupigwa mawe mpaka kufa. Hivyo
waliogopa sana hukumu hiyo kwa hiyo walipokuwa bado katika kipindi hicho. Maria
Mtakatifu alimweleza Yoseph kuwa alipendelea kuishi Maisha ya Ubikira na Utawa
mpaka kufa, Yoseph aliposikia maneno hayo alifurahi sana naye akasema mpendwa
wa moyo wangu tumshukuru Mungu kwa neema alizotujalia kwa kutukutanisha wenye
nia moja, kwani hata mimi nilikwisha jitolea kwa Mungu kuwa Mtumishi wake tangu
nikiwa na umri wa miaka kumi na miwili (12), basi nakuomba tuishi kama wachumba
katika maisha yetu yote.
Bikira
Maria aliposikia maneno hayo alifurahi sana, waliishi kitawa kila mmoja katika
chumba chake cha kulala hasa waliohamia Nazareti, wakiheshimiana na kusaidiana
kazi mbalimbali.
BIKIRA
MARIA ANATOKEWA NA MALAIKA GABRIEL
Katika
kipindi cha miezi sita na siku kumi na saba za kuishi baada ya ndoa yao, Maria
Mtakatifu alitokewa na Malaika Gabriel alitumwa na Mungu aende kwenye mji
uitwao Nazareti huko Galilaya kwa Msichana mmoja aitwae Maria, Mchumba wa mtu
mmoja jina lake Yoseph wa ukoo wa Daudi, Malaika akaingia nyumbani mwake akamwambia
"Salamu Maria, Umejaliwa neema nyingi, Bwana yu pamoja nawe" Maria
aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza maneno haya yana maana gani?
Malaika akamwambia "Usiogope Maria kwa maana Mungu amekujalia neema, ni
hivi; utapata mimba utazaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu".
Yeye
atakuwa Mkuu na ataitwa Mwana wa yule aliye juu, Bwana Mungu atampa kiti cha
Mfalme Daudi Babu yake. Kwa hiyo atautawala ukoo wa Yakobo milele na utawa wake
hautakuwa na mwisho. Maria akajibu, yawezekanaje hayo, hali mimi ni Bikira?
Malaika akamjibu "Roho Mtakatifu atakushukia na uwezo wake yeye aliye juu
utakujia kama kivuli kwasababu hiyo Mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu na
Mwana wa Mungu. Ujue pia kwamba hata Elizabeth jamaa yako naye amepata mimba
ingawa ni mzee na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa
tasa kwa maana hakuna lisilowezekana kwa Mungu." Maria akasema, "Mimi
ni Mtumishi wa Bwana nitendewe kama ulivyosema". Kisha Malaika akaenda
zake. Bikira Maria baada ya kusikia ujumbe huo wa Mungu hakumueleza Mmewe
ikabaki siri yake. Alikumbuka alivyoelezwa na roho Mtakatifu akiwa bado yupo
utawani, kuwa asimwambie mtu yeyote. Hivyo akayatunza maneno hayo yote moyoni
mwake.
YOSEPH
ANAGUNDUA MIMBA YA MARIA
Mimba
ilipotimiza miezi mitano Yoseph ndipo alipogundua alishangaa sana kwa sababu
alishindwa kujua ni jinsi gani Maria alivyoweza kuwa hivyo, kwani aliamini kuwa
Maria alikuwa ni Binti mwenye tabia nzuri tena mwenye kulinda usafi war oho
yake, alijiuliza uliza sana imekuaje! Kuna nini basi. Akajisikia uchungu Moyoni
mwake akahofia hukumu ya kuuwawa kwa kupigwa mawe, kwa kuvunja sheria na mila
za nchi yao.
Yote
yakamsibu na kumfanya afikiri namna itakavyokuwa, atakapofikishwa mbele ya
Kuhani na wazee wa mji hatimaye akapanga kutoroka lakini kabla ya kutimiza
hadhima yake hiyo aliamua kumuomba Mungu amjulishe jinsi Maria alivyopata mimba
hiyo akasema, "Mungu wangu, Mungu wa Ibrahim na Mungu wa Isacka kwani
ninayo hakika binti huyu hakufanya mapenzi na mtu yeyote siku zote amezishika
na kuzitimiza sheria za kitawa ila naamini kuna namna flani ya ukweli
iliyotendeka" alisubiri Mungu amjibu ombi lake. Akaendelea kumtunza Maria
kama kawaida naye Maria akawa Msichana mwenye upole sana, msikivu mwenye tabia
nzuri ajabu asiye na wasiwasi wote usiokuwa na mawaa.
Mambo
hayo Yoseph yalimshangaza sana.
Kwa
kawaida mwanamke anayepata mimba nje ya ndoa huwa na wasiwasi mwingi lakini
msichana huyu hata siku moja hakuonekana hivo……..
Mwisho.
Maoni
Chapisha Maoni