IBADA KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU
IBADA
KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU
SALA KABLA YA KOMUNIO – SALA YA
KUUTULIZA MOYO MTAKATIFU WA YESU
Ee
Yesu wangu, Mungu wangu na Bwana wa maisha yangu, sasa nataka kupokea komunio
Takatifu, ili nikurudishie mapendo na kukufariji kwa ajili ya ubaridi wote na
dhambi zote unazokosewa na watu katika Sakramenti hii ya mapendo. Ee Yesu,
nakuomba unipe nguvu niishike na niishi nia hili. Nami najua ya kwamba wewe
utakumbuka na kutimiza ahadi ya maneno uliyomwambia mtakatifu Margeth Maria
Alacok, kwamba: “Utakuwa kimbilio langu katika maisha yangu na hasa saa ya kufa
kwangu. AMINA”
Moyo
wa Yesu matumaini yao wanaokufa katika neema yako – Utuhurumie.
Moyo
wa Yesu malipo kwa dhambi zetu – utuhurumie.
AMINA.
1. SALA YA KUMWOMBA ROHO MTAKATIFU
AYAGEUZE MAISHA YETU.
Ee
Roho Mtakatifu, upendo na uzuri, uchangamfu, wa Baba na Mwana, maua na harufu
ya utakatifu wa Mungu. Moto Mtakatifu uliowashwa ndani yangu, uufanye moyo
wangu uwe mpya, yasafishe madoa yote, ondoa giza, teketeza uchafu wote na
uniumbie sura takatifu ya mwanao. Ewe Roho unayewaka na upendaye kukaa kwangu
pekee ili uweze kunitakatifuza , washa moto huu wa mapendo, uingie moyoni
mwangu na uingize na mwali wako wa moto. Ondoa mambo yote yenye nia mbaya na
mipango mibaya. Nipe nguvu ya kuwa mtume awezaye kutekeleza kazi yako. Nipe
neema ya kuwa mwali wa moto na uwake kwangu katika hali ya usafi wa moyo na
upendo. Ee Mungu wangu, ninakusadiki kwa maana wewe ndiwe ukweli wenyewe.
Ninakutumaini kwa maana wewe ni mwenye huruma isiyo na mwisho. Ninakupenda kwa
Moyo wangu wote na zaidi ya vitu vyote, kwa sababu wewe ni Mkamilifu kabisa na
nifundishe pia kumpenda na jirani yangu kama nafsi yangu kwa mapendo yako.
Ninazijutia dhambi zangu zote kwa moyo wangu wote kwa sababu zimekuchukiza wewe
uliye mwema sana. Kwa uthabiti nisikuchukize tena kwa neema yako.
AMINA
2. SALA YA KUUABUDU MOYO
MTAKATIFU WA YESU KATIKA EKARISTI TAKATIFU
Kwa nguvu zangu zote za
moyo wangu ninakuabudu. Ee Moyo Mtakatifu, na wa mwabudiwa sana, Moyo Mtakatifu
wa Bwana wetu Yesu Kristu, mimi nataka kukupenda na kukusalimu kwa usikivu
wote. Nipe neema yako ili nisikuudhi tena kwa sababu wewe ni mwema sana, Ee
Moyo Mtakatifu sana, nisaidie kukupenda kwa moyo wangu wote, nisaidie kukupenda
kuliko vitu vyote, nikupende kwa nguvu zangu zote na nikupende kwa uwezo wangu
wote. Nisaidie nichukie kweli dhambi na uovu wote, ninatamani kuwa mali yako
wewe uliyejitoa msalabani kwa ajili yangu kwa mateso makali.
Unionee huruma kwani mimi
mdhaifu na usiniruhusu kupotea kamwe. Ninajitolea kabisa kwako ee Moyo wa
mapendo kwa makusudi kwamba, utu wangu, maisha na mateso yangu yawe kwa ajili
ya kukupenda, kukuheshimu na kukutukuza wewe sasa, siku zote hata milele.
Ninakupenda ee moyo mwabudiwa wa Mwokozi wangu, ninaomba kwako uamuru moyo
wangu na kila kitu ndani yangu kikutukuze sana na milele.
AMINA.
3. SALA YA KUJIANDIKA
RAFIKI WA MOYO MTAKATIFU WA YESU
Mimi…………………….. sitaki
kujitumikia mimi mwenyewe bali ulimi wangu, macho yangu, masikio yangu, na
mwili wangu mzima, uwe na kazi ya kuuheshimu kuupenda na kuusifu moyo Mtakatifu
wako Ee Yesu Kristu. Ee Bwana Yesu, nakupa chochote kilicho changu. Yaani nafsi
yangu, muda wangu, mali zangu, maisha yangu, mateso yangu, pamoja na masumbuko
na mateso yote yatakayonipata katika maisha yangu. Leo, najifunga kwa sharti la
kuwa rafiki yako mwaminifu na mwanao wa kweli, nikitenda matendo yangu yote kwa
ajili ya kukupendeza wewe, nisaidie kukikataa katika maisha yangu chochote
kitakachokuchukiza wewe.
Ee Moyo Mtakatifu,
nakuelekea kwa kusudi moja tu, nalo ni upendo wangu kwako, uwe mlinzi wa roho
yangu. Uwe mlinzi wa maisha yangu. Uwe hakika ya wokovu wangu. Uwe dawa ya
udhaifu na unyonge wangu. Uwe mwenye kuponya vilema vyote vya maisha yangu. Na
uwe makimbilio yangu salama, hasa saa ya kufa kwangu.
Ee Moyo mwema, saa ya kufa
unioshe na kunitakasa kwa damu yako Takatifu ili nisiende kulaaniwa na Mungu
Baba, Aliye na haki ya kunikasirikia. Ee Moyo wa upendo, mimi naweka tumaini
langu lote kwako, kwa maana mimi naogopa kila kitu kwa ajili ya ubaya na
udhaifu wangu, lakini natumaini kila kitu kwa upendo wako. Uniondolee basi kitu
chochote kiwezacho kukuchukiza au kunizuia kuwa rafiki wa kweli na mwanao
mwaminifu, maana mimi nataka heri yangu, furaha yangu na sifa yangu yote iwe
katika kuishi na kufa kama rafiki yako mwaminifu na mwanao mpenzi.
AMINA.
4. LITANIA YA MOYO
MTAKATIFU WA YESU
Bwana utuhurumie, Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie, Kritu utuhurumie
Bwana utuhurumie, Bwana utuhurumie
Kristo utusikie, Kristu utusikilize
Baba wa Mbinguni Mungu, Utuhurumie
(Kiitikio
ni hicho kila baada ya Aya )
o
Mwana Mkombozi wa dunia Mungu
o
Roho Mtakatifu Mungu
o
Roho Mtakatifu Mungu mmoja
o
Moyo wa Yesu, Mwana wa Baba wa Milele
o
Moyo wa Yesu, uliotungwa na Roho
Mtakatifu
mwilini mwa Mama Bikira
o
Moyo wa Yesu, ulioungana na Neno wa Mungu.
o
Moyo wa Yesu, ulio na utukufu pasipo mfano
o
Moyo wa Yesu, hekalu takatifu la Mungu
o
Moyo wa Yesu, hema la Yule aliye juu
o
Moyo wa Yesu, nyumba ya Mungu na mlango wa
Mbingu
o
Moyo wa Yesu, tanuru yenye kuwaka mapendo.
o
Moyo wa Yesu, chombo cha haki na upendo
o
Moyo wa Yesu, unaojaa upendo na wema
o
Moyo wa Yesu, kilindi cha fadhila zote.
o
Moyo wa Yesu, unaostahili sifa zote
o
Moyo wa Yesu, unaotawala mioyo yote
o
Moyo wa Yesu, zinamokaa hazina za hekima na
elimu
o
Moyo wa Yesu, mnamokuwa utimilifu wote wa
Mungu
o
Moyo wa Yesu, uliopendelewa sana na Mungu
Baba
o
Moyo wa Yesu, uliotuenezea maziada yake
o
Moyo wa Yesu, mtamaniwa wa vilima vya Milele
o
Moyo wa Yesu, wenye uvumilivu na huruma
nyingi
o
Moyo wa Yesu, tajiri kwa wote wenye kukuomba
o
Moyo wa Yesu, chemchemi ya uzima na
utakatifu
o
Moyo wa Yesu, malipo kwa dhambi zetu
o
Moyo wa Yesu, ulioshibishwa matusi
o
Moyo wa Yesu, uliovunjika kwa sababu ya
ubaya wetu
o
Moyo wa Yesu, uliotii mpaka kufa
o
Moyo wa Yesu, uliochomwa kwa mkuki
o
Moyo wa Yesu, chemchemi ya faraja zote
o
Moyo wa Yesu, uzima na ufufuo wetu
o
Moyo wa Yesu, Amani na upatanisho wetu
o
Moyo wa Yesu, sadaka ya wakosefu
o
Moyo wa Yesu, unamokaa wokovu wao wenye
kukutumainia
o
Moyo wa Yesu, matumaini yao wenye kuzimia
kwako Moyo wa Yesu, sababu ya furaha kwa watakatifu wote
………………………………
Mwana kondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi
Za dunia Utusamehe Bwana,
Mwana kondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi
Za dunia Utusamehe Bwana,
Mwana kondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi
Za dunia Utusamehe Bwana,
K.
Yesu Mwenye Moyo Mpole na Mnyenyekevu
W.
Ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako.
Tuombe:
(W)
Ee Mungu, Mwenyezi wa milele uuangalie Moyo wa Mwanao mpendelevu, pia na heshima
na malipo aliyokutolea kwa ajili ya wenye dhambi, uridhike, uwaondolee wenye
kuomba toba kwako kwa njia ya huyo mwanao Yesu Kristo, anayeishi na kutawala
nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu daima na milele.
5. SALA YA MALIPIZI KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU
Ee Yesu mpendelevu, unayewapenda
mno watu, hata wasio na shukrani, wenye kuzembea na kukudharau. Tutazame sisi
tunaojinyenyekesha chini ya Altare, tuna hamu ya kufanya malipizi kwa heshima
ya pekee kwa ukatili wa wewe kupuuzwa na majeraha ambayo moyo wako Mpendelevu
unatiwa na kuumizwa na watu popote
Ee Yesu, hata sisi
tumehusika katika kushiriki kukuudhi na kukuletea uchungu mwingi. Kweli
tunaujutia na kuusikitikia moyoni mwetu. Tunakiri makosa yetu na kukuomba kwa
unyenyekevu msamaha, tukikujulisha kuwa tu tayari kufanya malipizi ya majuto na
kitubio, bila ya kulazimishwa, siyo tu kwa ajili ya wale walio nje ya njia ya
wokovu, wale wanaokataa kukufuata wewe Mchungaji na kiongozi wao, lakini pia
kwa wale wasiojali maagano ya ubatizo wao, lakini pia kwa wale wasiojali
maagano ya ubatizo wao, wakitupilia mbali nia njema ya amri yako wakishika mila
na desturi za kiafrika zinazokataliwa na Injili, wanaoshika imani za kipagani,
wanaoendekeza ushirikina, wanaoendekeza sadaka kwa mizimu, kupiga ramli na matambiko.
Sasa
tuna kusudi la kutoa fidia na kufanya malipizi ya makosa kwa namna ya pekee,
hasa zaidi kwa makosa haya:
1. Ya
kukosa heshima katika mioyo vitendo na vishawishi vingi vinavyofanywa duniani
kwa kuwanasa na kuwadanganya watu wanyoofu.
2. Kwa
kutohudhuria Ibada za jumapili na siku zilizoamriwa.
3. Kwa
kufuru za kuchukiza wanazosema watu juu yako, juu ya Mama yetu Bikira Maria, na
juu ya watakatifu wako.
4. Kwa
matusi juu ya Baba Mtakatifu na mapadri wako.
5. Kwa
uzembe na kufuru ambazo Sakramenti yako ya Ekaristi inatumiwa vibaya sana
katika ulimwengu wa leo.
6. Mwisho,
kwa madhambi yote ya wanadamu ya kukataa na kupinga haki na mamlaka ya
mafundisho ya kanisa lako uliloliweka.
Laiti
kama ingaliwezekana kuosha kwa damu zetu maovu na machukizo ya aina hii. Na
sasa katika ukaidi na ujeuri huo unaofanywa dhidi ya heshima yako ya kimungu
tunapenda kutoa sadaka ile uliyotoa Msalabani kwa Baba yako na ambayo unaifanya
tena kila siku katika Altare zetu. Tunapenda kuitoa tukiunganisha na malipizi
ya Bikira Maria nay a watakatifu wote na ya waumini wote hapa duniani – wale
wenye mapenzi mema.
Tunaahidi
kweli, kulipa kadiri tunavyoweza kwa uzembe tunaoufanya kwa mapendo yako makuu
kwa dhambi ambazo sisi na wengine tumezitenda zamani, kulipa kwa imani thabiti
na maisha safi na kwa kutimiza amri ya mapendo nay a jirani, tunaahidi pia
kuzuia wengine kadri tuwezavyo, wasikuchukize na pia kuwafanya watu wengine
iwezekanavyo kukupenda na kukufuata.
Ee
Yesu mpendelevu, kwa maombezi ya Bikira Maria aliye mfano katika kufanya malipizi,
tafadhali pokea tendo letu hilo la hiari la malipizi na ukitupatia zawadi ya
uvumilivu, tutakuwa waaminifu mpaka kufa katika wajibu wetu na utii kwako, ili
sisi sote tuyafikie yale maskani yetu ya heri na furaha unapoishi wewe pamoja
na Baba na Roho Mtakatifu mkitawala daima na milele.
AMINA.
7.
ROZALI
YA MOYO MTAKATIFU WA YESU
(Kwenye Msalaba)
Ee
Yesu utupe moyo wako kama amana ya upendo wako na kimbilio letu, ili tupate
pumziko salama wakati wa maisha yetu na faraja tamu saa ya kufa kwetu. Amina.
·
Baba yetu
·
Salamu Maria tatu
·
Atukuzwe baba
·
Nasadiki
(Kwenye kila tendo)
Ninakuabudu,
ninakutukuza na ninakupenda ee Moyo wa Yesu wangu mpenzi, uliopenywa na huzuni
kwa ajili ya dhambi ambazo zimekuwa zikitendwa hata leo dhidi ya Sakramenti
takatifu sana ya Altare, ninakutolea hapo kwa kuuridhisha pia, moyo wa Mama
yako mpendevu Bikira Maria, na kwa mastahili ya watakatifu wote. Amina.
(Kwenye chembe za Salama Maria – zile
50)
Ee
Moyo Mtakatifu wa Yesu uwakao mapendo wetu
- Uwashe
nyonyo zetu kwa upendo wako.
8.
NOVENA
KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU
1.
Ee Yesu uliyesema “kweli nawaambieni, ombeni
nanyi mtapewa, tafuteni nanyi mtapata, gongeni nanyi mtafunguliwa”, tazama
ninagonga, ninatafuta na kukuomba neema ya ……………………
Baba yetu…………… Salama Maria …………………
Atukuzwe Baba…………
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu,
ninakutumainia kwa moyo wangu wote.
2.
Ee. Yesu uliyesema “Kweli nawaambieni,
chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu atawapeni”, tazama kwa jina lako
ninakuomba neema ya………………..
Baba Yetu……………. Salamu Maria……………..
Atukuzwe Baba………
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu,
ninakutumainia kwa moyo wangu wote.
3.
Ee Yesu uliyesema “kweli nawaambieni, mbingu
na dunia zitapita lakini maneno yangu hayatapita kamwe” tazama, nikitiwa nguvu
na ukweli wa maneno yako haya, ninakuomba
Neema ya …………………….
Baba Yetu…………………….. Salamu Maria
……………….
Atukuzwe Baba ……………..
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu,
ninakutumainia kwa moyo wangu wote.
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu,
ambao kwako ni kitu kimoja tu kisichowezekana, yaani kutoacha kuwaonea huruma
wenye huzuni, utuhurumie sisi wakosefu na maskini na utujalie neema
tulizokuomba kwa njia ya Moyo Imakulata wa Bikira Maria, Mama yako na mama yetu
mpole.
Malizia kwa kusali:
“Salamu Malkia” na malizia:
“Mt. Yosefu Baba Mlishi wa Yesu, utuombee” x 3
4. SALA YA MAOMBI
Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu,
ninakukimbilia, ninakuja kwako katika mikono yako yenye huruma. Ndiwe tegemeo
langu na tumaini langu thabiti. Ndiwe mwenye dawa ya maovu yangu yote, malipizi
ya makosa yangu yote. Waweza kunipatia haja zangu na neema ninazoziomba mimi na
wanazoziomba wengine. Wewe upo ili kutusaidia sote, ndiwe mwanga mkuu
usiozimika kamwe, ndiwe chanzo cha nguvu, uvumilivu, amani na faraja yetu.
Nina hakika kuwa maombi
yangu hayatakuchosha nawe hutaacha kunisaidia, kunilinda na kunipenda, kwani
wewe Yesu upendo wako hauna mwisho. Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu unihurumie,
uyasikilize maombi yangu, kadiri ya huruma yako. Nawe katika sisi, na kwa ajili
yetu, ufanye lolote unalohitaji, kwani tunajitoa kwako kwa imani na uhakika
thabiti kwamba kamwe hautatuacha, sasa hata milele.
AMINA.
9.
SALA
KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU KUOMBA KUTIMIZIWA AHADI
Ee
Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ututazame sisi tunaopiga magoti mbele yako ili
kukuabudu, kukusifu, kukushukuru, kufanya malipizi kwa makosa ya zamani
tukikumbuka ahadi ulizoahidi, tunathubutu kusema kwa matumaini yetu yote.
(K)
Moyo Mtakatifu wa Yesu tujalie neema zote zilizo za lazima katika hali zetu za
maisha.
Kiitikio: umeahidi Ee Bwana.
Moyo
Mtakatifu wa Yesu tuletee amani nyumbani mwetu na katika jamaa zetu.
Kiitikio:……
Moyo
Mtakatifu wa Yesu tufariji katika taabu, mateso na maisha yetu yote.
Kiitikio………..
Moyo
Mtakatifu wa Yesu, uwe Makimbilio yetu salama katika maisha hasa saa ya kufa
kwetu.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu tushushie Baraka na neema nyingi katika kazi na shughuli zetu
zote.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu fanya wakosefu wote wapate katika Moyo wako kisima na habari
isiyo na mwisho ya huruma yako.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu fanya mioyo iliyo baridi, vuguvugu na legevu kuwa na bidii na
hodari mwingi
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu fanya roho zilizo na bidii kuendelea kukamilika katika
utakaso na utakatifu.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu bariki mahali panapowekwa kwa heshima sanamu ya Moyo wako
katika nyumba zetu.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu wape mapadri na wale wanaoshughulikia wokovu wa roho za watu
nguvu na uwezo wa kuigeuza hata mioyo migumu.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu andika na yasifutwe milele, majina ya wale wote wanaoanzisha,
kueneza na kusali Ibada hii wao wenyewe na kwa watu wengine.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu tujalie kwa huruma ya moyo wako, sisi na wengine tutakaopokea
komunio Takatifu Ijumaa ya kwanza ya mwezi kwa miezi tisa mfululizo neema ya
kutubu tusife maadui wako wala kufa bila kupokea Sakramenti. Moyo wako uwe
makimbilio yetu salama saa ile ya mwisho.
Kiitikio ……………
Moyo
Mtakatifu wa Yesu fanya ufalme wako wenye nguvu utufikie ingawa shetani na
jitihada za adui wako zinapinga vikali sana.
Kiitikio ……………
TUOMBE: Ee
Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunaweka matumaini yetu yote kwako. Ingawa mambo mengi
yanatutisha sababu ya udhaifu wetu. Lakini bado tunatumaini mambo yote katika
wema na huruma yako. Tunakusihi, uwe peke yako mapendo yetu yote, Mlinzi wa
maisha yetu yote, nguvu katika udhaifu wetu wote na ukweli katika matendo na
maneno yetu yote. Uwe shahidi wa wokovu wetu na makimbilio yetu wakati wa kufa
kwetu. AMINA.
…………………………….
Maoni
Chapisha Maoni