SALA KWA AJILI YA KUFUNGULIWA KUTOKA KATIKA NGUVU ZA GIZA
SALA KWA AJILI YA KUFUNGULIWA KUTOKA KATIKA NGUVU ZA GIZA
Ifuatayo
ni Sala nzuri sana kwajili ya mtu anayeshumbuliwa na nguvu za giza, Sala hii
imeambatana na masharti au Muongozo tu awali ambao unakuwandaa vema kusali sala
hii.
Na
unapoanza kusali, Isali kwa kumaanisha na inapotokea unashindwa kusali wewe
anayeweza aendelee kusali kwa niaba yako.
o Upande wa maombi kumbuka kila siku kurudia maombi yako yale
yale mpaka Mungu atakapo kujibu
o Upande ya sehemu ya ahadi inayoambatana na maombi yako,
kumbuka ahadi hizo unaingia wewe na Mungu wako, ikitokea umevunja ahadi zako
kaungame haraka kwa Mungu wako.
o Mwisho Sali Rozali ya huruma ya Mungu na ………
MASHERTI
YA SALA HIZI
1. Anza Sala hizi kwa kuungama kwanza dhambi zako zote
tangu ulipokuwa na ufahamu, (ungama hata dhambi ambazo ulikuwa umeishaungama
zamani)
2. Baada ya hilo, omba misa maalumu, isomwe kwa nia yako. Usipokuwa
na pesa basi itolee tu kimoyomoyo misa ambayo itakuwa ni kwa ajili ya kuanza
rasmi kuzisali sala hizi. Wakati wa misa toa maombi maalumu ya kuomba unachotaka na kuahidi kuwa ukipewa
unachotaka utamtolea Mungu kitu gani (Ahadi hizi ni kama kuishi vizuri katika
ndoa au kama mtu hana ndoa kuishi utakatifu wa kweli, yaani kuachana kabisa na
dhambi kama ngono, kutupilia mbali maswala ya ushirikina, utoaji wa mimba kwa
wanawake na yote ambayo dhamiri yako inaona ni machukizo kwa Mungu)
Ikumbukwe nguvu ya sala si katika maneno anayosali mtu
bali ni matendo yake. Unapoomba neema maalumu kasha ukaishi ovyo ovyo kwa
madhambi ni sawa na kumtukana Mungu. Matokeo si tu kuwa hutapata unachokiomba bali
utasababisha pia hasira ya Mungu. Hata hivyo kwa tuko binadamu, si rahisi ukawa
mtakatifu siku moja. Dhambi ndogo ndogo kama hasira, uvivu, kuwasengenya watu –
hizi zitakuwepo. Lakini wakati wote wa sala hizi jikumbushe kuungama mara kwa
mara, ili maisha yako yawe na Baraka ya kuweza kupokea unachokiomba.
3. Pamoja sala hizi, kila siku Sali sala ya rozari ya
kawaida ikiambatana na sala zilizoandikwa. Sala hizi siyo lazima zifuatane.
Zinaweza kusaliwa kwa vipindi tofauti, La muhimu lazima zisaliwe zote kila
siku. Rozari kuanza nayo, au kuisali baada ya sala hizi. Mwisho wa sala hizi
imeandikwa Rozari ya Huruma ya Mungu. Hiyo ndiyo inahitimisha jumla ya sala
hizi. Hizi ni sala ndefu lakini zenye nguvu ya uponyaji ajabu.
4. Jitahidi kufunga walau mara moja kwa wiki muda wote
unaposali sala hizi funga kwa kujinyima chochote utakachokimudu. Mfano, funga
chakula, yaani ule mara moja kwa siku, au funga kuangalia televisheni, au siku
hiyo Sali muda mrefu sana, na kadhalika. Kama una mashaka jinsi na namna gani
ufunge kumuuliza padre yoyote akupe mwongozo. Hata hivyo kumbuka mafungo ya
maana Zaidi ni kuacha dhambi. Hilo ni sharti muhimu sana kupata unachoomba
5. Katika kipindi chote hiki uwe mtu mwadilifu kadiri ya
uwezo wako wote. Epuka dhambi yoyote kubwa au ya makusudi. Kama ulishiriki
chochote kwa kufahamu au kutofahamu kinachohusu mambo ya ushirikina, matambiko,
au madawa yanayokatazwa na kanisa hakikisha unayaacha kwa roho yote kabisa,
kabisa, kabisa. (Kanisa linakubali dawa asilia za kawaida tu. Endapo una
mashaka kama dawa fulani inaruhusiwa au vipi basi, pata ushauri kutoka kwa
padre)
6. Ufahamu kuwa unaposali sala hizi siku za mwanzo kitakuwa
ni kipindi cha majaribu mengi. Maana yake ni kwamba shetani anataka kukukatisha
tamaa. Yashinde yote kwa nguvu ya sala, na Imani. Utakapokuwa unaendelea,
magumu yataanza kupungua. Magumu haya ninayosema ni kwa mfano: Unaweza kujikuta
una hasira sana, au una usingizi wa ajabu, au kuugua ugua, wengine wanaposali
sala hizi huwa hadi wanatapika, wengine tumbo linawauma sana, ndoto za ovyo na
kadhalika. Haya yote ukikazana na kuzama zaidi na Zaidi yataisha.
7. Sali sala hizi kwa mfululizo kila siku hadi Mungu
atakaposikiliza ombi lako. Usihesabu umesali wiki ngapi au miezi mingapi. Jambo
muhimu ni kuwa usizisali kama unasoma gazeti. Zama kwa moyo wako wote na kwa
Imani yako yote kabisa. Ukijua wazi kuwa uko mbele ya Mungu na kuwa unapambana
na shetani. Iweke nafsi yako yote kwa unyenyekevu wako wote mbele ya Mungu.
Siri ya uponyaji iko hapo. Na usiwe na mashaka yoyote kabisa.
8. Ukiweza kila unapopata uwezo omba misa kwani sala ya
misa ndiyo sala kubwa kuliko zote. Omba misa mara nyingi kadri utakavyoweza. Na
hata usipoiomba misa, katika kipindi chote kila uingiapo kanisani, ombi lako
liwe hilo hilo la nia uliyoweka. Hukatazwi pia kuongeza nia zingine, lakini nia
kubwa iwe hii. ……………………………….
SALA KWA AJILI YA KUFUNGULIWA KUTOKA KATIKA NGUVU ZA
GIZA
1. KWA JINA LA YESU
Katika Jina la Yesu wa Nazareti, Baba wa Mbinguni,
ninakuinulia mkono wangu wa kuume. Mimi mwanao, ……. ( hapa taja jina lako)
Nitazame Bwana maana nguvu na uwezo wote unatoka kwenye
kiti chako cha enzi. Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya 62:11-12 "Mara moja amenena Mungu, mara mbili
nimeyasikia haya, ya kwamba nguvu zina Mungu. Na fadhili ziko kwako ee Bwana,
maana ndiwe umlipaye mtu sawa sawa na haki yake "
Baba wa Minguni, ninapokea nguvu kutoka kwako sasa kwa
jina la Yesu. Ninatumia nguvu hizi kufuta, kuvunja, kuharibu na kujitenga
mwenyewe kutoka kwenye laana zote za maagano yaliyofanywa dhidi yangu. Ninaamuru
laana zote pamoja na mapatano na mazindiko yaliyojificha popote dhidi maisha
yangu kujidhihirisha sasa katika jina la Yesu. Ninaamuru moto wa Roho Mtakatifu
na damu ya Yesu kuwadhihirisha wote. Ninaziharibu nguvu zenu zote kwa jina la
Yesu – AMINA.
Baba yetu uliye Mbinguni x 10. Salamu Maria x 10, KISHA
Atukuzwe Baba x 3.
2. DHAMBI NA LAANA ZA
WAHENGA WANGU.
Katika jina lenye nguvu na uwezo la Bwana wetu Yesu
Kristo wa Nazareti, ninatubu dhambi zilizofanywa na wahenga wangu. Laana ya
hizo dhambi zinaniandama hadi leo mimi. Ninavunja na kuharibu laana zote,
maagano na matambiko kutoka kwa mababu zangu, hata kama laana hizo
zimesababishwa na uovu wowote walioufanya. Ninaziharibu kwa jina la Yesu Kristo
wa Nazareti – AMINA.
Naziharibu na kuzivunja laana zote, mapatano na
matambiko katika upande wa Baba yangu na Mama yangu katika Jina la Yesu. Bila
kujali ni haina gani ya laana iliyowekwa juu yangu. Bila kujali ni maagano gani
wahenga wangu wamefanya na shetani, na bila kujali ni wapi wamefanya mambo ya
matambiko na mazindiko juu yangu: iwe ni angani, duniani au baharini.
Ninayaharibu yote kwa jina la Yesu – AMINA.
Pia ninavunja laana, maagano na matambiko niliyofanyiwa
na Baba yangu, Mama yangu na wazazi wao (Babu na Bibi) kutoka kizazi chochote
kwa upande wa Baba yangu na Mama yangu bila kujali laana, matambiko, mazindiko,
mapatano na ushirikiano wao wote kuwa yalifanyika wapi. Ninaamuru yote
kuvunjika na kuharibiwa katika jina la Yesu Kristo – AMINA.
Baba Yetu Uliye Mbinguni x 10. Salamu Maria x 10, KISHA
Atukuzwe Baba x 3
3. KUTOKA KWANGU
MWENYEWE
Katika Jina la Yesu ninakwenda kinyume na laana zote
nilizozisababisha mimi mwenyewe juu ya maendeleo yangu ya maisha yangu kwa
kujua au kutojua.
Ninakuvunja wewe laana popote pale ulipojificha. Iwe
angani, duniani au baharini. Ninaharibu na kuzivunja nguvu zako zote katika
Jina la Yesu. Ninakuja kinyume na maagano niliyoyafanya na miungu na pepo
wachafu, maruhani, majini, majini bahari, waume wa kipepo, wanawake wa kipepo,
watoto wa kipepo na mizimu. Iwe katika ulimwengu huu au ulimwengu wa kiroho au
hata katika ndoto.
Ninavunja maagano yote katika jina la Yesu. Mazindiko yote
niliyojifanyia nayo ninaharibu yote. Ninajiondoa katika mazindiko hayo.
Ninalifuta jina langu kutoka katika kitabu cha shetani. Ninajitangazia uhuru
leo katika jina la Yesu. Ninajifunika kwa damu ya Yesu kristo wa Nazareti –
AMINA.
Baba Yetu uliye Mbinguni x 10. Salamu Maria x 10, KISHA
Atukuzwe Baba x 3.
4. KWA KUTOMTII MUNGU
Ninaziungama na kuzitubu dhambi zangu kwa jina lako
Baba. Katika jina la Yesu ziondoe laana zote juu yangu kwa ajili ya kutozitii
amri zako. Umkemee yule aliye katika maisha yangu, kama ilivyoandikwa katika
kitabu cha Malaki 3:8-12 "Ondoa zinge, tunutu na viwavi kutoka
kwangu" Ninyeshee mvua za mwanzo na za mwisho. Nijaze tena Baraka zako,
katika jina la Yesu – AMINA.
Baba Yetu uliye Mbinguni x 10. Salamu Maria x 10, KISHA
Atukuzwe Baba x 3.
5. KUJITENGA NA
ULIMWENGU
Baba wa mbingu, ninajishusha na kujitenga na Ulimwengu
na vishawishi vyake na laana zake zote. Najitenga tena na maagano na mazindiko
yote niliyofanyiwa na niliyoyafanya, kwa kufahamu au kwa kutofahamu. Mimi niko
huru sasa. Na kwa tamko la kinywa change sasa, namchagua Bwana wangu Yesu
kristu tangu leo kuwa Bwana na Mfalme wangu. Tangu sasa mimi ni kiumbe kipya.
Roho Mtakatifu yu juu yangu sasa. Na tangu sasa nayaweza yote katika jina la
Yesu Kristo anitiaye nguvu. Ninamwaibisha shetani sasa na ninamtangazia uhuru
wangu katika jina la Yesu Bwana wangu. Ninaharibu mipango yote ya shetani aliyo
nayo juu ya maisha yangu. Popote anapojificha, ninaamuru moto wa Roho Mtakatifu
umuunguze usiku na mchana hata milele kwa jina la Yesu – AMINA
Baba Yetu Uliye Mbinguni x 10. Salamu Maria x 10, KISHA
Atukuzwe Baba x 3.
6. KUJIFUNIKA KWA DAMU
YA YESU
Najifunika sasa kwa damu ya Kristo, ninajilowesha mimi
mwenyewe. Ninaifunika nyumba na chumba ninamoishi, Nawafunika majirani zangu
wabaya, naifunika kazi yangu, naifunika mipango yangu yote na nakifunika kila
nilicho nacho. AMINA
Damu ya Kristo – Nioshe,
Damu ya Kristo – Nitie nguvu,
Damu ya Kristo – Niburudishe,
Damu ya Kristo – Uwe juu yangu,
Damu ya Kristo – Uwe chini yangu,
Damu ya Kristo – Uwe nyuma yangu,
Damu ya Kristo – Uwe mbele yangu,
Damu ya Kristo – Uwe ndani yangu,
Damu ya Kristo – Unikinge
Damu ya Kristo – Unipiganie,
Damu ya Kristo – Uniimarishe dhidi ya mwovu,
Damu ya Kristo – Unilinde dhidi ya vishawishi
AMINA.
7. KUOMBA NEEMA MAALUMU
1. Yesu wangu, wewe ulituahidi kwamba: `Ukweli nawaambia,
ombeni mtapewa, tafuteni mtaona, na bisheni hodi mtafunguliwa, `Nami kwa Imani
kubwa nabisha hodi, natafuta na naomba neema ya …….. (taja ombi lako)
Baba Yetu………………………. Salaamu
Maria ……………. Atukuzwe Moyo Mtakatifu wa Yesu, Nakuamini na najiaminisha kwako.
2. Yesu wangu, uliyesema:- "Ukweli nawaambieni,
chochote muombacho kwa Baba yangu kwa jina langu, Yeye atawapeni," Nami,
kwa kutaja jina lako Takatifu, naomba neema ya …………… (Rudia ombi ulilotaja juu)
Baba yetu …………………………….
Salaamu Maria …………….. Atukuzwe Baba Moyo Mtakatifu wa Yesu, Nakuamini na
najiaminisha kwako.
3. Yesu wangu uliyesema, :- " Mbingu na dunia
zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe," Nami nikijiaminisha kwa
ahadi ya maneno hayo matakatifu naomba neema ya …….. (Rudia mara ya tatu ombi
ulilotaja)
Baba yetu …………………………
Salamu Maria …………………….
Atukuzwe Baba …………………..
Moyo
Mtakatifu wa Yesu, Nakuamini na najiaminisha kwako.
4. Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambao kamwe hauwezi kuacha
kutuhurumia sisi wakosefu, tuhurumie wanao wakosefu, na tujalie neema
tulizokuomba kupitia kwa Moyo safi wa Bikira Maria, ambaye ni mama yako na Mama
yetu pia.
Ee
Mtakatifu Yosefu , Baba Mlishi wa Familia Takatifu Utuombee..
(Rudia
mara tatu maneno hayo)
8. AHADI
Ili kupata neema hii ya …………………. Na pia iambatane na
kufunguliwa Baraka zote kutoka mbinguni, name nakuahidi Mungu wangu kuwa na
mwenendo mwema kweli wa Kikristo. Kubeba msalaba wangu kama anavyoniagiza Yesu
na kuishi kwa kuangalia mbingu kila siku. Najiweka mimi mwenyewe chini ya
usimamizi wa Mama Bikira Maria mama mwenye usafi kamili wa moyo na mama yangu
tangu sasa nikimwahidi kuishi maisha safi ya Kikristo, kwa unyenyekevu kasha,
nakukabidhi maisha yangu yote. Nakuahidi (1) kutunza usafi wa moyo (2)
kutojihusisha na nguvu za giza hadi kufa (3) kudumu katika sala. Naomba tangu
sasa maisha yangu yote yafunikwe tena na damu ya Yesu yenye Baraka na nguvu
isiyoshindwa sasa hadi saa ya kufa kwangu – AMINA
9. LITANIA YA HURUMA YA
MUNGU
Bwana utuhurumie ……………………….
Kristu utuhurumie …………………………
Bwana atuhurumie ……………………….
Kristu utusikie ………………… Kristu utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu….. Utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu ……….. Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja ………….. Utuhurumie
v Huruma ya Mungu iliyo sifa kuu ya Muumba wetu ……………….
TUNAKUTUMAINIA
v Huruma ya Mungu iliyo kilele cha Ukamilifu wa mwokozi
wetu,
v Huruma ya Mungu iliyo upendo usiopimika wa Roho
Mtakatifu.
v Huruma ya Mungu iliyo fumbo kuu la utatu Mtakatifu.
v Huruma ya Mungu iliyo ishara ya uwezo Mkuu wa Mungu
Mwenyezi,
v Huruma ya Mungu iliyoonyeshwa katika kuziumba Roho za
Malaika,
v Huruma ya Mungu iliyotuumba na kutufanya tuwepo,
v Huruma ya Mungu inayoushika na kuuhuisha ulimwengu
mzima,
v Huruma ya Mungu inayotujalia maisha ya kutokufa,
v Huruma ya Mungu inayotukinga na adhabu tunazostahili,
v Huruma ya Mungu inayotufanya wenye haki, katika neno
aliyejifanya mtu.
v Huruma ya Mungu inayofurika kutoka katika Majeraha ya
Kristo,
v Huruma ya Mungu inayobubujika kutoka ndani ya Moyo
Mtakatifu wa Yesu,
v Huruma ya Mungu aliyotupatia Bikra Maria Mtukufu kabisa
awe kwetu "Mama wa Huruma"
v Huruma ya Mungu inayoonyeshwa katika ufunuo wa Mafumbo
Matakatifu ya Mungu,
v Huruma ya Mungu ilionyeshwa katika kuanzisha kanisa Katoliki
v Huruma ya Mungu inayopatikana katika mafumbo ya
Sakramenti Takatifu.
v Huruma ya Mungu inayotolewa kwa wanadamu wote kwa njia
ya ubatizo na kitubio,
v Huruma ya Mungu inayotolewa katika Sakrameti ya Ekaristi
na daraja takatifu,
v Huruma ya Mungu inayoonekana katika uongofu wa wakosefu,
v Huruma ya Mungu inayoonyeshwa katika kuwatakatifuza watu
wenye haki,
v Huruma ya Mungu chemchem ya afya kwa wagonjwa na wote
wanaoteswa,
v Huruma ya Mungu iliyo faraja ya wote wenye uchungu
moyoni,
v Huruma ya Mungu iliyo tumaini la roho zinazokata tamaa,
v Huruma ya Mungu iliyo mwenzi wa daima na popote wa watu
wote.
v Huruma ya Mungu inayotuletea neema zote.
v Huruma ya Mungu iliyo Amani yao wanaokufa.
v Huruma ya Mungu iliyo tumaini na faraja ya marehemu
Toharani.
v Huruma ya Mungu iliyo furaha ya Mbinguni kwa watakatifu
wote,
v Huruma ya Mungu iliyo taji la watakatifu wote,
v Huruma ya Mungu chemchemi ya miujiza ya daima.
Mwanakondoo
wa Mungu, uliyetuonyesha huruma yako kuu katika kuikomboa dunia kwa msalaba
wako Mtakatifu,
W. UTUSAMEHE BWANA.
Mwanakondoo
wa Mungu, anayejitolea kwetu kwa mapendo na Huruma katika kila adhimisho la
sadaka ya misa Takatifu,
W. UTUSAMEHE BWANA.
Mwanakondoo
wa Mungu unayeondoa dhambi za dunia kwa njia ya huruma yako isiyo na mwisho.
W. UTUHURUMIE
Bwana
utuhurumie……. Bwana utuhurumie
Kristu
utuhurumie……. Kristu utuhurumie
Bwana
utuhurumie….. Bwana utuhurumie.
………………………..
Ee
Damu na Maji, yaliyobubujika kutoka katika Moyo wa Yesu kama chemchemi ya
huruma kwetu…… TUNAKUTUMAINIA
………………………..
Tuombe
Ee
Mungu uliye na huruma isiyo na mwisho, na hazina za wema na upendo wako hazina
mipaka, tunakusihi, ututazame sisi watu wako huku duniani na kutuongezea huruma
yako tena na tena, ili itusaidie, tusije tukakata tamaa hata mara moja, hata
tunapokumbana na majaribu makubwa kiasi gani, bali tuweze daima kuzielekea na
kuzishika amri zako kwa Imani, matumaini, na mapendo na kutimiza daima mapenzi
yako Matakatifu, ambayo ndiyo Huruma Yenyewe.
Tunaomba
hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao, Mfalme wa Amani na Huruma, aishiye
na kutawala Nawe na Roho Mtakatifu, kwa pamoja mkituonyesha Huruma isiyo na
mwisho, daima na milele.
Amina.
TAZAMA VIDEO HII KUJIFUNZA ZAIDI
Maoni
Chapisha Maoni