NOVENA KWA MAMA BIKIRA MARIA MPALIZWA MBINGUNI

 


NOVENA KWA MAMA BIKIRA MARIA MPALIZWA MBINGUNI

v  SEKWENSIA

 

1.    Uje Roho Mtakatifu,

Tuangaze toka mbinguni,

Roho zetu kwa mwangao.

 

2.    Uje Baba wa maskini,

Uje mtoa wa vipaji,

Uje mwanga wa mioyo.

 

3.    Ee Mfariji mwema sana,

Ee rafiki mwanana,

Ee raha mustarehe.

 

4.    Kwenye kazi u pumziko,

Kwenye joto, burudisho,

U mfutaji wa machozi.

 

5.    Ee mwanga wenye heri,

Uwajaze waamini,

Neema yako mioyoni.

 

6.    Bila nguvu yako wewe,

Mwanadamu hana kitu,

Kwake yote yana kosa.

 

7.    Osha machafuko yetu,

Panyeshee pakavu petu,

Na kuponya majeraha.

 

8.    Ulegeze ukaidi,

Pasha moto wa ubaridi,

Nyosha upotevu wote.

 

9.    Wape waumini wako,

Wenye tumaini kwako,

Paji zako zote saba.

 

10. Wape tuzo ya fadhila,

Wape mwisho bila hila,

Wape heri ya milele.

 

11.  Amina aleluya,

Amina aleluya,

Amina aleluya.

 

2. SALA YA MWANZO

Bwana Yesu Kristu, umeishinda nguvu ya kifo na kutujalia tumaini la maisha ya milele. Ulimjalia Mama yako nafasi ya pekee katika utukufu wako, na hukuruhusu uharibifu uguse mwili wake. Tunapofurahi katika kupalizwa mbinguni Bikira Maria, tuimarishe katika ushindi wa maisha dhidi ya kifo AMINA.

Nia za Novena:

i.             Kwa ajili ya amani ya ulimwengu

Ee Mama mpenzi Bikira Maria Mpalizwa mbinguni tunaweka nchi yetu na Ulimwengu mzima chini ya ulinzi wako wa Ki-mama, utuombee tujaliwe Amani.

 

ii.           Kwa ajili uongofu wa wakosefu

Kwa maombezi yako Ee Mama Mpalizwa mbingu, Mwenye Huruma, wakosefu wapate neema na mwanga wa kugeuza mawazo na mienendo yao, wajaliwe toba ya kweli, wachukue hatua za kuelekea kupata huruma ya Mungu.

 

iii.          Kwa ajili ya Kanisa

Tunaaliombea Kanisa Takatifu la Mungu, uliangalie na kulilinda liendelee kutumulikia nuru na mwanga wa kutuangazia katika safari yetu ya kumwendea Mungu.

 

iv.          Kwa ajili ya viongozi wa Kanisa

Tunawaweka mikononi Mwako Ee Mama Mpalizwa mbinguni; Baba Mtakatifu, Maaskofu, Mapadre na watawa, Mungu awaimarishe na kuwajalia neema ili kwa njia ya uongozi wao roho nyingi zifike kwa Mungu.

 

v.            Kwa ajili ya Familia

Tunakutolea familia zetu Ee Mama Bikira Maria, Malkia wa familia, tujaliwe fadhila za amani, matumaini na upendo. Kwa maombezi yako ee Mama mpole kila mwanafamilia atambue wajibu wake na kuutimiza kwa mapendo na utukufu wa Mungu.

 

vi.          Kwa ajili ya utume wa walei katika Kanisa.

Mama na Mwalimu wa Yesu Kristu, kwa mapendo ya mama, uvilee, uvielekeze, uvitunze, uvilinde, uvistawishe, uviongoze na kuviimarisha vyama vyote ya kitume ndani ya Kanisa. Na kwa maombezi yako Ee Mama mpenzi waumini wote tujaliwe mwamko wa utume na kutimiza vyema wajibu wetu katika kanisa.

 

vii.        Kwa ajili ya Mwenye shida.

Bikira na Mama, tunawaombea wagonjwa wapone, wakosefu watubu, waasi warudi nyumbani kwa Baba. Na marehemu wa toharani warehemiwe wapumzike kwa amani.

 

Tuombe: (Kadiri ya siku)

 

Siku ya kwanza:

Bikira mwenye moyo safi, Mama wa Bwana wetu Yesu Kristu na Mama yetu, tunaamini katika kupalizwa kwako kwa ushindi mbinguni, ambako Malaika na watakatifu wanakutukuza kama Malkia wa mbingu nan chi. Tunaungana nao katika kukusifu, na tunamtukuza Mungu aliyekuinua juu ya viumbe vyote. Pamoja nao tunakuheshimu. Tuna hakika kwamba unasimamia maisha yetu ya kila siku na tunakuomba utusaidie sasa. Tunatulizwa na imani yetu katika ufufuko ujao na tunategemea sala zako na kitulizo. Baada ya maisha ya hapa duniani, utuonyeshe Yesu mzao wa tumbo lako. Ee mpole, Ee mwema, ee mpendelevu Bikira Maria.

Malkia uliyepalizwa mbinguni, tuombee Amina.                   

 

Siku ya pili

Bikira Maria uliyepalizwa mbinguni, tunakuheshimu kama Malkia wa mbingu na nchi kama ulivyoonja machungu ya maumivu na mateso ya Mwanao hapa duniani, sasa unafurahia faraja ya milele pamoja naye mbingu. Tunamsifu Bwana wetu Yesu Kristu kwa kutupa sisi Mama mpendelevu kama wewe.

Malkia uliyepalizwa mbinguni, tuombee. Amina

Siku ya tatu

Ewe Mama uliyepalizwa mbinguni, kwa kuwa ulishiriki mafumbo yote ya ukombozi wetu, Yesu amekutuza Utukufu. Kwa nguvu ya maombi yako tusaidie Ee Mama mpendelevu kuwasilisha shida zetu kwa Yesu Bwana wetu.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

Siku ya Nne

Mama mpendwa Maria uliyepalizwa mbinguni, Mungu alikuwekea mkono wake wa kulia, ili uweze kuwasaidia watoto wake, kama Mama wa Mungu. Katikati ya watakatifu unasimama kama Malkia wao na wetu, karibu na Mungu kuliko kiumbe chochote. Unawaombea watoto wako na kutujalia kila Baraka aliyojipatia Mkombozi wetu juu ya msalaba. Tafadhali tusaidie katika mahitaji yetu na muombe Bwana Yesu atujalie tunayoomba iwapo ni kwa manufaa ya roho zetu.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

 

Siku ya tano

Ewe Mama mpendelevu na mwenye huruma, tunaomba utukufu na uzuri wako viijaze mioyo yetu, chukizo dhidi ya malimwengu, na ari kubwa ya furaha ya mbinguni. Macho yako ya huruma yaangaze chini kwenye mapambano na madhaifu yetu katika hili bonde la machozi. Basi Mama mpendelevu, sikia ombi letu na msihi Bwana Yesu kwa ajili yetu. Tuvishe vazi lako safi la upendo na neema hapa, na umilele na utukufu mbinguni

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

Siku ya sita

Maria, Mama yetu mpendwa na Malkia Mkuu, chukua na pokea mioyo yetu maskini, pamoja na utashi na matamanio yake, pamoja na neema na Baraka inayoweza kujaliwa. Yote tulivyo, na yote tunayoweza kuwa, yote tuliyo nayo katika hali ya asili na ya neema tumepokea kutoka kwa Mungu kwa njia ya msaada wako. Tusaidie Mama, tumkabidhi Mungu yote, pamoja na maombi yetu. Mama yetu na Malkia, katika mkono yako mitakatifu tunayaweka yote.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

Siku ya saba

Bikira Maria, Malkia wa kila moyo, pokea yote tulivyo, na utufunge kwa Yesu kwa vifungo vya upendo ili tuwe wako milele, natuweze kusema kwa ukweli “Mimi ni wa Yesu kupitia kwa Maria.”

Mama Yesu uliyepalizwa mbinguni, na Malkia wa ulimwengu, Bikira daima, Mama wa Mungu, tupatie tunayoomba, iwapo ni kwa sifa na utukufu wa Mungu na kwa faida ya roho zetu. Mama yetu uliyepalizwa mbinguni tunakupenda. Tujalie upendo zaidi kwa Yesu na kwako.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

Siku ya nane

Mama Maria uliyepalizwa mbinguni, tuna furaha kwamba wewe ni Malkia wa mbingu na dunia. Umempa Mungu “nitendewe ulivyonena” yako na kuwa Mama wa Mkombozi. Tuombee amani na wokovu kwa njia ya sala zako, kwa kuwa umemzaa Kristu Bwana wetu mwokozi wa wanadamu. Hivyo basi tupelekee shida zetu mbele ya kiti cha enzi.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

Siku ya tisa

Mbarikiwa Mama uliyepalizwa mbinguni, baada ya miaka ya ushahidi – bingwa hapa duniani tunafurahi kwamba hatimaye umefikishwa kwenye kiti ulichotayarishiwa mbinguni na utatu Mtakatifu. Inua mioyo yetu katika utukufu wa kupalizwa kwako, mbali na machafu na madoa ya dhambi. Tufundishe jinsi dunia ilivyo ndogo inapotazamwa kutoka mbinguni. Tuwezeshe kuelewa kwamba kifo ni mlango wa ushindi ambao tutapitia kufika kwa Mwanao na kwamba siku moja miili yetu itaunganika na roho zetu katika heri ya milele mbinguni.

Kutoka duniani humu tunamopita kama mahujaji, tunautegemea msaada wako. Kwa heshima ya kupalizwa kwako mbinguni tunaomba utusaidie. Saa ya kifo chetu tuongoze kwa usalama hadi kwa Yesu, kuufurahia uso wa Mungu kwa milele yote pamoja na wewe. Tuombee tustahilishwe ahadi za Kristu.

Malkia uliyepalizwa mbinguni utuombee. Amina.

3. ROZARI YA UTUKUFU

4. LITANIA YA MAMA BIKIRA MARIA

5. MATOLEO / WIMBO

6. WIMBO

(k) Ishara kubwa imeonekana mbinguni x 2

Mwanamke aliyevikwa jua (pia) na mwezi chini ya miguu yake,

Na taji la nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake x 2

 

1.    Tufurahie sote katika Bwana / tunapoadhimisha siku kuu kwa heshima ya Bikira Maria.

2.    Jeshi la Malaika washangilia / pia wafurahia kupalizwa mbinguni kwake Bikira Maria.

3.    Bwana amefunua wokovu wake kati ya mataifa / ameidhihirisha haki yake juu yao.

4.    Atukuzwe Baba pia na Mwana na Roho Mtakatifu / kama mwanzo sasa na siku zote na milele.

 

TUNAKIMBILIA ULINZI WAKO… / WIMBO

 

Imeandaliwa na

Mtumishi: Julius Mmbaga

 

 


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAHAMU JINSI YA KUOMBA SALA YA VITA

IBADA KWA MOYO MTAKATIFU WA YESU

CHANGAMOTO YA NDOTO KATIKA ULIMWENGU WA ROHO

MALAIKA MKUU MT. MICHAEL UTULINDE KATIKA VITA

SALA KWA AJILI YA KUFUNGULIWA KUTOKA KATIKA NGUVU ZA GIZA

HISTORIA YA MAISHA YA BIKIRA MARIA