TOHARANI NI WAPI NA INAPATIKANA WAPI KWENYE BIBLIA?
TOHARANI NI WAPI NA INAPATIKANA WAPI KWENYE BIBLIA?
(Naomba ni
kushirikishe kusoma habari hii nzuri juu ya Toharani ambayo nimeikuta mahali
bila kupunguza au kuongeza neno naomba Tusome pamoja tujifunze kitu.
• Iko hivi...
Kwa mujibu wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Toharani inaelezwa
kama Utakaso wa mwisho (final purification). Yaani wale wote waliokufa katika
Huruma ya Mungu, na urafiki na Mungu. Lakini hawakuwa Safi kabisa, lazima
waende kwanza Toharani ili wakatakaswe kabla ya kuingia Mbinguni.
Ile hali ya Utakaso kabla ya kuingia Mbinguni, ndio tunaiita
"Toharani" na fundisho hili linaadhimishwa rasmi ndani ya Kanisa
kupitia Mitaguso ya Florence na Trent. (Rejea Catechism Of The Catholic Church
1030-31).
Kamusi ya Concise Oxford inaeleza neno
"Toharani" kama eneo, sehemu au hali ya mateso inayopata roho
za wenye dhambi ndogo kama malipizi yake, ili itakasike kabla ya kuingia
Mbinguni.
"A place or state of suffering inhabited by the souls of
sinners who are expiating their sins before going to Heaven".
Kwa Kingereza Toharani hujulikana kama "Purgatory",
kwa Kilatini ni "Purgatorium".
Maneno yote haya yana maana moja kuwa, ni eneo la Utakaso kwa
roho zenye dhambi nyepesi kabla hazijaingia Mbinguni.
Neno "Toharani" au "Purgatory" halipo kwenye
Biblia, iwe ya tafsiri ya Kiswahili au English version n.k
Hali kadhalika hata neno lenyewe "Biblia" halipo
kwenye Maandiko Matakatifu, yaani Biblia yenyewe haijataja kama inaitwa
"Biblia".
Vile vile neno "Utatu" au "Trinity" hauwezi
kulipata sehemu yoyote ile kwenye Biblia, lakini haimaanishi kwamba hakuna
fundisho linalotupa tusiamini uwepo wa Utatu Mtakatifu.
Kwahiyo neno kutotajwa kwenye Biblia, haifanyi neno hilo
lisiwepo. Kwani pale Biblia haijapataja, basi Mapokeo yana kitu cha kutuambia.
Hakika Biblia ilibuniwa ili kuyataja yale Maandiko Matakatifu
yaliyojumuishwa pamoja. Vivyo hivyo neno "Toharani" limebuniwa ili
kuwakilisha eneo au hali ambayo zile roho zilizotenda dhambi nyepesi
zinapelekwa pale ili kutakaswa kabla ya kuingia Mbinguni.
Fundisho kuhusu Toharani limetajwa kwenye Biblia katika Kitabu
cha pili cha Wamakabayo na Injili ya Mathayo.
Kumbuka, neno "Toharani" halipo ila
"Concept" kuhusu Toharani ipo.
Ukatoliki haujajengwa tu kwa Maandiko Matakatifu (Sola
Scriptura), bali pia katika Mapokeo Matakatifu.
Kwani kupitia Maandiko na Mapokeo Matakatifu, ndipo misingi ya
mafundisho ya Kanisa Katoliki yanapatikana.
*CONCEPT AU FUNDISHO KUHUSU TOHARANI TUNAIPATA WAPI KWENYE
BIBLIA?*
Nini tunakipata katika Kitabu cha pili cha Yuda Makabayo, moja
ya vitabu vinavyopatikana tu kwenye orodha ya vitabu vya Biblia Takatifu.
Deuterocanonical books ambapo Waprotestanti wanakiweka kwenye
orodha ya vitabu vya "Apocrypha" yaani "Vitabu visivyokubalika".
Basi naomba rejea 2Makabayo 12:39-45 inasema:
39. Siku iliyofuata waliona ni haraka na muhimu kukusanya miili
ya wenzao waliokuwa wameuawa vitani, na kuizika katika makaburi ya wazee wao.
40. Lakini katika kila maiti, walikuta zimefichwa nguo sanamu
ndogo ndogo za miungu iliyoabudiwa yamnia, jambo ambalo sheria inawakataza
Wayahudi kuzivaa. Hapo kila mtu alijua ni kwanini hao walikuwa wameuawa.
41. Hivyo wakazisifu njia za Bwana Hakimu mwenye Haki, afichuaye
vilivyofichika.
42. Na wakamwomba Bwana afutulie mbali dhambi hiyo, kisha Yuda
yule mtu mwadilifu akawataka watu waepuke dhambi, kwa sababu walikuwa
wamejionea wenyewe yaliyokuwa yamewapata wale waliokuwa wametenda dhambi.
43. Pia alichangisha fedha kutoka kwa watu wake, fedha ipatayo
drakma elfu mbili akaipeleka Yerusalem kwa ajili ya dhabihu ya kuondoa dhambi.
Yuda alifanya tendo lililo jema, kwa sababu aliamini katika ufufuo wa wafu.
44. Kama asingekuwa na imani kwamba wafu watafufuliwa, ingekuwa
ni upambavu na kazi bure kuwaombea marehemu.
45. Lakini akiwa anatazamia tunzo nzuri walioekewa waliokufa
wakiwa waaminifu kwa Mungu, hilo lilikuwa wazo jema na takatifu. Kwahiyo Yuda
alitolea dhabihu ya upatanisho, ili wote wapate kuondolewa dhambi zao.
Myahudi Yuda Makabayo alifanikiwa kuongoza vita dhidi ya Mfalme
Antrochus IV wa Syria, kati ya mwaka 167 - 160 BC.
Baadhi ya maaskari wake walifia vitani, katika kupekua maiti zao
ndipo Yuda na wenzake wakagundua kuwa, baadhi ya wale maaskari waliokufa
walikuwa wamevaa visanamu vya bahati viunoni na shingoni, tuseme ni kama yale
makonokono ya baharini, ambazo baadhi yetu tunawavalisha watoto wetu, eti
kuwakinga na watu wenye macho mabaya.
Sasa Hawa Askari walivaa visanamu vya miungu yamnia kama kinga
yao wasiuawe vitani.
Katika sheria ya Torati ya Musa na Amri za Mungu, hii ilikuwa ni
kosa kubwa mno kwa Wayahudi kwa kuwa Amri ya kwanza ya Mungu iliwakataza
kufanya hivyo.
Kiufupi askari hawa walikuwa wametenda dhambi, japo walikuwa
katika mapambano ya kutetea imani yao, watu watu na taifa lao la Israel kwa
ujumla.
Kwahiyo baada ya Yuda kuona hivyo, hakuwaacha bali alifanya sala
ya toba kwa ajili yao, na hata kutoa dhabihu ya maondoleo ya dhambi zao. Kitu
alichokifanya Yuda, ndicho kinachofanywa na Wakatoliki hadi leo.
Hebu pia angalia Mathayo 12:32, inasema:
32. Tena asemaye neno la kumpinga Mwana atasamehewa, lakini yule
asemaye neno la kumpinga Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu huu wala
ule ujao.
Hapa Yesu anasema nini? Kwamba dhambi zote zitasamehewa, ila ile
ya kumkufuru Roho Mtakatifu haitasamehewa kwenye ulimwengu huu (duniani) wala
ule ujao (toharani).
Kwa tafakari ya kina Yesu anatuambia kwamba, kuna maondoleo ya
dhambi sehemu mbili, katika ulimwengu huu na ule ujao.
Huo ulimwengu ujao ambao kuna maondoleo ya dhambi ni upi? Biblia
haijatupa jina, lakini kupitia Mapokeo Matakatifu ya Kikatoliki sisi tumeuita
ni "Toharani".
Kumbe basi kama dhambi zako hazikuondolewa katika ulimwengu huu
wakati ulipofariki, kuna uwezekano zikaondolewa katika ulimwengu ujao. Ikiwa
itafanyika Ibada ya maombezi kama ile aliyoifanya Yuda Makabayo, kwa wale
maaskari wake waliofia vitani.
Ikumbukwe, Yesu anasema sio kila dhambi itaondolewa kwenye
ulimwengu ujao (Toharani), kama dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.
Mtu kama yupo motoni (hell) hakuna sala itakayomfikia, kwani
kuna ukuta mkubwa sana kati yetu na wao. (Luka 16:25-26).
Lakini kama mtu huyo yuko Mbinguni (Heaven) hakuna sala
inayohitajika juu yake. Lakini kama sasa ikitokea mtu huyu hastahili kwenda
motoni wala kuingia Mbinguni, moja kwa moja kuna sehemu atakwenda kwanza,
sehemu hiyo anaweza kuombewa kama Yuda Makabayo alivyofanya.
Sasa kwanini sehemu hiyo tusiipe jina? Kama ilivyo Mbinguni na
motoni, sehemu hii nayo inastahili kupewa jina la utambulisho.
Kanisa Katoliki limepaita mahali hapo kuwa ni Toharani. Jina
hili halipatikani mahali popote, lakini Mapokeo Matakatifu yanatuambia panaitwa
Toharani.
Mapokeo Matakatifu yanatuambia kuwa, Toharani sio sehemu ya
kungojea hukumu au sehemu ya kifungo, bali ni mahali pa Utakaso kabla ya
kuingia Mbinguni.
Mafundisho ya Kanisa Katoliki yanasema kuwa, Toharani sio chumba
cha mateso, bali ni kama chumba cha maandalizi kabla ya kuingia Ikulu ya Mfalme
Yesu Kristo.
Dhambi kubwa hukumu yake ni kwenda jehanamu, ila dhambi nyepesi
ambazo hazikutendwa kwa makusudi, utakaswa Toharani.
Amini kwamba, Toharani ipo na ni fundisho halali la Kikatoliki
linaloonesha kukubalika bila mashaka yoyote (dogma), lakini fundisho kuwa kila
roho lazima ipite Toharani kabla ya kwenda Mbinguni hilo sio fundisho la Kanisa
Katoliki.
Fundisho la Toharani lilipewa mkazo zaidi na Papa Gregory Mkuu
(590 - 604 AD) Kanisa Katoliki lilifafanua fundisho hili na kuliweka rasmi
katika Baraza la Lyons (1274), na Baraza la Florence (1439) na lilakazaniwa
zaidi kwenye Baraza la Trent (1547). Kumbuka Baraza ndio Mtaguso kwa jina
lingine.
Paulo aliwauliza Wakorintho (1Kor 15:29) kuwa:
29. Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya
wafu wanatumaini kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa
ajili yao?
Kumbe mtazamo wa Mtume Paulo na Yuda Makabayo juu ya kuwaombea
wafu, walikuwa sahihi kwa watu wote waliotumaini juu ya ufufuo wa wafu.
Paulo anaendelea kusema (1Kor 3:13-15) kuwa:
13. Iwe iwavyo ubora wa kazi ya kila mtu mmoja utaonekana wakati
siku ile ya Kristo itakapoifuchua. Maana siku hiyo itatokea moto, na huo moto
hutapima na kuonesha ubora wake.
14. Ikiwa alichojenga mtu juu ya huo msingi, kitastahimili huo
moto, atapokea tuzo.
15. Lakini kama alichojengwa kitaunguzwa, basi atapoteza tuzo
lake. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
Rejea ule mstari wa 15 unaosema: "Inaweza ikawa ulichojenga
kikaunguzwa, yaani haukustahili kupewa tuzo, lakini bado ukaolewa kwa mithili
ya kuponyoka.
Hii ina maana kuwa, sio wote watakaonekana kuwa wenye dhambi,
basi wataenda motoni, wako ambao watakaonekana. Kwa tafakari ya kina, hao
watakaoponyoka ni wale ambao roho zao ziko Toharani.
Aya hii ya 15 unaweza ukaielewa zaidi kama utaisoma tena kwa
tafsiri ya Kingereza:
"If anyone's work is burned up, he will suffer loss, though
he himself will be saved, but only as through fire" (1Cor 3:15).
Kwa maelezo haya machache, naamini utakuwa umenielewa.
*RAHA YA MILELE UWAPE EE BWANA...*
Maoni
Chapisha Maoni