SIMULIZI ZA KWELI KUHUSU TOHARANI.
SIMULIZI ZA KWELI KUHUSU TOHARANI.
Toharani
ni mahali pa mateso, lakini ndani yake kuna furaha na matumaini makubwa ya
kumuona Mungu siku moja.
Roho
zilizoko Toharani ni tofauti kabisa na sisi tuliokuwa hai angali bado tuko
duniani, kwa sababu tunaishi tu bila kuwa na uhakika kama tutamuona Mungu baada
ya kufariki.
Kwa
mujibu wa Katekisimu ya Kanisa Katoliki inasema: Toharani ni mahali pa Utakaso,
ambapo mtu mwenye dhambi ndogo ndogo anapokufa, basi hulazimika kwanza kuingia
Toharani kutakaswa kabla ya kwenda Mbinguni.
Hivyo
ni jukumu letu la kila siku kama Kanisa linalosafiri hapa duniani, kuwasaidia
hawa wenzetu katika sala, Ili wapate neema ya haraka katika kushiriki furaha ya
Pasaka huko Mbinguni. Kwani roho zilizoko Toharani, wanahitaji sana sala zetu.
*1. MTAKATIFU PADRE PIO*
Simulizi hii ni ya kweli iliyotokea
kule Italy, linaonesha wazi kwamba, roho zilizoko Toharani daima wanahitaji
sana sala zetu Ili watoke huko.
Siku moja mnamo mwaka 1920,
Mtakatifu Padre Pio alipokuwa akisali katika lofti ya kwaya, ghafla alisikia
sauti ya ajabu kutoka kwenye Altare ya Kanisa.
Ilikuwa ni sauti ya Candelabra,
kijana mdogo sana wa makamo, ikianguka kutoka kwenye Madhabahu kuu. Padre Pio
alipomuona, Kijana yule akamwambia:
"Baba, ninafanya malipizi yangu
hapa Toharani, maana nilikuwa mwanafunzi katika seminari hii. Sasa nahitaji
kurekebisha kwa makosa niliyoyafanya wakati nilipokuwa hapa, kwa sababu ya
uvivu wangu wa kufanya kazi za Kanisa kwa ulegevu".
Pia inasemekana kwamba, kijana huyo
alikuwa Toharani takribani miaka 60, na baada ya kuomba maombi kutoka kwa Padre
Pio, alipotea na kurudi Toharani.
Roho nyingine nyingi sana kutoka
Toharani, zinasema kwamba: Baada ya kuomba msaada wa Padre Pio, basi alitumia
usiku mzima katika sala akiwaombea. Na hivyo Mungu kupitia sala zake,
aliwahurumia na kuwaruhusu kuingia Mbinguni.
*2. MTAKATIFU THERESA WA AVILA*
Mtakatifu huyu alikuwa ni Mtawa wa
Shirika la Wakarmeli, na inasemekana kwamba ndiye Mwanzilishi wa shirika hilo
akishirikiana na Mtakatifu Yohane wa Msalaba.
Mtakatifu Theresa wa Avila naye
alisema kwamba: Baada ya kujua kuwa Padre wake alikuwa amekwisha kufa, basi
Mungu akamwambia, Padre huyo atakuwa Toharani hadi Misa itakaposomwa katika
Kanisa la nyumba mpya ya Wakarmeli itakayojengwa.
Kwa haraka Mtakatifu Theresa
alikwenda kwenye eneo la ujenzi na kutafuta wafanyakazi, kwa ajili ya kuanza
kazi ya kuinua kuta za Kanisa mara moja.
Lakini kwa kuwa iliweza kuchukua
muda mrefu kukamilika, basi aliomba ruhusa kutoka kwa Askofu kwa ajili ya
kujenga Kanisa la muda mfupi.
Kanisa lilipokamilika, Misa
iliadhimishwa hapo. Na wakati alipokuwa anapokea Sakramenti ya Ekaristi
Takatifu, Mtakatifu Theresa aliweza kuona maono ya Padre yule akimshukuru kwa
neema alizozipata kwake kabla ya kuingia katika Ufalme wa Mungu.
*3. MTAKATIFU ELIZABETH WA URENO*
Mtakatifu huyu ambaye alitawala
Ureno kama Malkia wa nchi yake, alikuwa na binti aliyempenda sana aitwaye
Constance.
Mtoto huyu mdogo alikufa ghafla
baada ya kuolewa, na kusababisha Malkia Elizabeth na Mumewe kupata huzuni
nyingi juu ya kifo chake.
Siku moja Hermit alimwendea Malkia
Elizabeth alipokuwa anasali, akamwambia habari ya kushtusha sana kwamba,
Constance alimtokea akimuomba achukue ujumbe kutoka kwa mama yake huku
akimueleza kuwa, sehemu aliko kule Toharani anateseka sana, na angeendelea kuwa
huko kwa muda mrefu zaidi.
Basi baada ya maelezo hayo, wakaamua
kuweka Misa Takatifu kila siku kwa ajili yake. Naye Constance kupitia maombezi
ya Malkia Elizabeth na watu wake wa karibu, aliweza kupata huruma ya Mungu na
kuruhusiwa kuingia Mbinguni.
Ndugu
yangu, hizi ni simulizi chache tu nimekuandalia ili uone Toharani ni sehemu pa
namna gani.
Kwani
Toharani haina utofauti na Jehanamu, kwa sababu zote zina moto. Lakini uzuri ni
kwamba, moto wa kule Toharani uko kwa ajili ya kuzitakasa roho kabla ya kuingia
Mbinguni.
Kwahiyo
Toharani sio mahali pa mchezo, na ndio maana Mama Kanisa ameweka mwezi huu wote
wa Novemba kwa ajili ya kuziombea Roho hizo zilizoko Toharani, ili kupitia sala
zetu, wapate neema ya haraka ya kutoka huko.
Kipindi
hichi cha Novemba, sio tu kwa ajili ya kuziombea roho zinazoteseka Toharani,
bali pia ni kwa ajili yetu wenyewe, tujitafakari baada ya maisha ya hapa
duniani tutakuwa wapi.
Hivi
ushawahi kujiuliza kwanini bado unaishi? Najua utakuwa hujui, ila ukweli ni
kwamba unaishi ili kwa sababu utumie muda wako vizuri katika kutenda mema na
kumtumikia Mungu siku zote, na ndio maana bado uko hai.
Siku
moja nlipokuwa Kwenye Misa nilimsikia Padre mmoja katika Mahubiri yake akisema
kwamba:
Watu
wema na wabaya hufa kwa sababu, wale waliokuwa wema wasiendelee kubaki duniani
wasije kuanguka dhambini na kukosa Ufalme wa Mbingu.
Pia
hata wale waliokuwa wabaya hufa mapema, ili wasisababishe wale waliokuwa wema
wakatenda dhambi na kupotea kwenye ziwa la moto wa milele.
Hivyo
kwa kuwa sisi bado tunaishi, ni wazi kwamba tuko katikati yaani sio watu wema
sana na wala sio wabaya mno. Kwahiyo tunaishi ili kujenga maisha yetu ya baadae
baada ya kuondoka hapa ulimwenguni.
Basi
pumzi tuliyonayo tuitumie vizuri katika kutenda mema, na sio kufanya mambo ya
anasa, zinaa, ulevi na yote yahusuyo dunia.
Ni
heri kufanya matendo mema hapa duniani, hata kama utakufa na usimuone Mungu,
hiyo haina shida. Kuliko ufe katika hali ya dhambi kubwa huku ukisema hakuna
Mungu, halafu baadae unakufa na ukamuona Mungu. Sijui itakuwaje.
Hivyo
mwezi huu ni mwezi wa kujitafakari juu ya maisha yetu wenyewe, kama kuna sehemu
tumekosea tujirekebishe. Pia tusisahau kuwaombea na wenzetu walioko Toharani,
maana walikuwa kama sisi tulivyo, na siku moja na sisi tutakuwa kama wao.
Sote
tu marehemu watarajiwa, tuishi vizuri katika Upendo na wenzetu, ili
tutakapokufa hapa dunia tuache alama nzuri ya kuigwa na siku moja tukapokee
tuzo ya Utakatifu huko Mbinguni.
Maoni
Chapisha Maoni