HISTORIA ZA WATAKATIFU

 

-Mtakatifu Adelaide wa Burgundy*

Mtakatifu Adelaide alizaliwa mwaka 931, huko Orbe, Upper Burgundy(Uswisi sasa). Alikuwa Binti wa Rudolf II wa Burgundy na Bertha wa Swabia.

Aliolewa akiwa na miaka 15 na Lothair  II ambaye alikuwa mtawala wa Italia.Lakini Lothair alikufa miaka 3 baadaye kwa kulishwa sumu,  katika kugombea utawala.Tayari katika ndoa yao walishapata mtoto mmoja wa kike aliyeitwa Emma.

Mtawala aliyefuata Berengar II, alijaribu kumlazimisha Adelaide kuolewa na mwanae aliyeitwa Adalbert. Lakini alikataa.Kutokana na hilo alifungwa jela kwa miezi 4.

Mtakatifu Adelaide alitoroka jela na kuomba hifadhi na ulinzi toka kwa mfalme Otto I.Wakafunga ndoa mwaka 951.

Mwaka 962 Papa John XII alimvisha Otto I taji la ufalme wa Italia, na Adelaide akiwa malkia. Wakapata watoto wanne.Mtoto wao mkubwa aliitwa Otto II.

Mwaka 973 mfalme Otto I alikufa na mwanae Otto II akatawala. Na mwaka 983 Otto II naye akafa.Mjukuu wa Adelaide aliyeitwa Otho III akatawala.  

Mtakatifu Adelaide alisimamia ufalme akingoja mjukuu wake kufikisha umri wa kutawala kwa miaka minne.  Na ilipotimia ,    alijiuzuru nyadhifa zote na kuamua  kumtumikia Mungu.

Mtakatifu Adelaide alienda kuishi katika manosteri ya Selz huko Alsace mwaka 991.Akajenga manosteri nyingine nyingi ,akasaidia wenye shida mbalimbali.

Mtakatifu Adelaide alikufa mwaka 999 Desemba 16 huko Seltz, Alsace (Ufaransa sasa).Alitangazwa mtakatifu mwaka 1097 na Papa Urban II.



Mama yetu Bikira Maria wa Guadalupe:

Tunakumbuka  mama yetu, Bikira Maria, jinsi alivyomtokea mkulima masikini aliyeitwa Juan Diego,  huko katika uwanda wa  Tepeyac, katika mji wa Mexico city, nchini Mexico, Jumamosi tarehe 9 Disemba 1531.

Katika tokeo hilo, Mama Maria, alimwagiza Juan Diego, akamwambie Askofu, kujengwe Kanisa mahali pale alipotokea. Juan Diego alipomweleza Askofu Juan de Zumárraga , neno hilo lilipokelewa kwa wepesi mno ili kumridhisha. Akiwa njiani kurudi nyumbani, Juan Diego alitokewa tena na Mama Maria, pale pale katika uwanda wa Tepeyac. Mama Maria, alimweleza kuwa aliamua kumtuma yeye, kwa kuwa alimchagua yeye kati ya watu wote.

Jumapili asubuhi, Desemba 10, Juan Diego alienda tena kanisani, akaomba kuonana tena na Askofu. Baada ya kumsikiliza tena, alimwambia kuwa aje na ushahidi wa maagizo ya kujengwa kwa kanisa katika uwanda  wa Tepeyac. Juan Diego alirudi tena na kutokewa tena na Mama Maria. Mama Maria  akamweleza kuwa atampa ushahidi huo.

Jumanne asubuhi, Desemba tarehe 12, 1531, Juan Diego alienda kanisani kumchukua Padri ili akampe mpako wa wagonjwa mjomba wake ambaye alikuwa mgonjwa sana. Kwa woga wa kutokewa tena na Mama Maria, alibadilisha njia, ili kukwepa asitokewe. Njia nyingine tena aliyopita,  alitokewa tena na Mama Maria. Juan Diego,  alimweleza Mama Maria kuwa anaenda kumchukua Padri ili akampe mjomba wake mpako wa wagonjwa. 

Mama Maria, alimwambia Juan Diego,  asihofu kuhusu mjomba wake, bali apande uwandani, achume maua (ambayo ni mazuri mno, na hayapatikani mwezi Disemba), ampelekee Askofu kama ushahidi. 
Juan Diego  alichuma maua na kuyaweka katika nguo yake ya kuzuia baridi (Tilma). Akaenda kwa Askofu na kumwonesha maua hayo kuwa ndio ushahidi aliopewa. 

Alipofungua nguo yake (Tilma) na kuyamwaga mezani maua, picha ya Mama Maria ikizungukwa na maua yale ilibaki katika nguo hiyo. Askofu na wote waliokuwa chumbani humo, walipiga magoti kwa heshima ya Mama Bikira Maria. 

Muda huo huo, Nyumbani kwa Juan Diego, mjomba wake aliyekuwa mgonjwa, aliyeitwa Juan Bernardino, alitokewa pia na Mama Maria, na kumwambia asiwe na hofu kwa kuwa amepona, na akajitambulisha kuwa yeye ni Bikira Maria wa Guadalupe.
Hii ndio historia.

Mwenye heri  Antony Grassi, Padre*
Mwenyeheri Antony Grassi alizaliwa mwaka 1592, November 13, huko Fermo, Marche Italia.

Alijiunga katika shirika la watawa wa Karmeli, hapo Fermo tarehe 11 October 1609 na akapata daraja la upadri  mwaka 1617 Desemba 17.

Mwaka 1621 wakati akisali katika kanisa dogo huko Loreto, alipigwa na radi ambayo iliunguza nguo zake na yeye kubaki salama.   

Mwaka 1625 alienda kuhiji huko Roma. Na mwaka 1635 alichaguliwa kuwa mkuu wa shirika. Alifanya kazi ya Mungu kwa bidii na upendo, na watu walimuita "malaika wa amani".

Mwenyeheri Antony Grassi alikufa kwa amani akizungukwa na watu wa shirika lake, pamoja na Askofu  wa Fermo, mwaka 1671 Desemba 13.

Alitangazwa mwenye heri mwaka 1900 September 30 na Papa Leo XIII.



*Mtakatifu Lucia Bikira na shahidi*

Mtakatifu Lucia , alizaliwa mwaka 283 huko Syracuse Italia.Baba yake alikuwa mkatoliki,  lakini alikufa wakati Lucia akiwa na miaka 5 tu.

Katika mji jirani wa Catania,kilometa 50 kutoka Syracuse,  kulikuwa na kaburi na kituo cha hija cha mtakatifu Agatha.Mama yake Lucia,  Eutychia, alikuwa akienda kusali mahali hapo ,pamoja na mwanae.

Kuna wakati mama Eutychia aliugua mno.Lucie akapata maono kutoka kwa mtakatifu Agatha kuwa mama yake angeponywa.Na muujiza huo ukatokea na akaponywa. Mtakatifu Lucia aliona kuwa ni nafasi nzuri kwake, kumshawishi mama yake ili wagawe baadhi ya vitu vyao kwa maskini.

Baada ya kugawa vitu, gavana wa Syracuse aliyeitwa Paschasius, alifahamu kuwa Lucia na mama yake, walitoa zawadi kwa ajiri ya kumshukuru Mungu.  Paschasius alichukizwa na hilo, na akamuamuru Lucia kutoa sadaka ya kuteketezwa mbele ya  sanamu ya mfalme. Lucia alikataa . Paschasius aliamuru atupwe jela.

Mtakatifu Lucia alipitia mateso makubwa , ikiwa ni pamoja na kutolewa macho.

Mtakatifu Lucia aliuwawa kwa kukatwa kichwa mwaka 304 huko Syracuse,  Italia.Hii ndio historia fupi ya Mt.Lucia.


*Mtakatifu  Bibiana, Bikira na Shahidi*

Mtakatifu  Bibiana,  alikuwa Binti wa Flavian, shujaa wa kirumi na mkewe Dafrosa, ambao walikuwa wakristo. 

Mwaka 363 , Mtawala wa dola ya kirumi, alimteua Apronianus kuwa gavana wa Roma. Gavana huyo alimkamata Flavian na baada ya mateso makali, alimpeleka uhamishoni, ambako alikufa. Mkewe Dafrosa  alikatwa kichwa.

Bibiana na dada yake aliyeitwa Demetria,  waliachwa katika umaskini mkubwa.Walikaa na njaa muda mwingi, wakisali na kuomba.Gavana Apronianus aliamuru  waletwe mbele yake . Demetria alipoulizwa kuamua imani yake, alikiri imani na kufa hapo hapo. 

Bibiana alikabidhiwa kwa mwanamke mmoja aliyeitwa Rufina.Rufina alimtesa mno na kumfanyia mabaya. Lakini hakukata tamaa, na mwisho , Apronianus aliamuru afungwe katika nguzo na kupigwa hadi kufa.






Mtakatifu Olyimpias*

Mtakatifu Olyimpias alizaliwa huko Constantinople ( Uturuki) kati ya mwaka 361 katika familia ya kitajiri. Baba yake aliitwa Seleucus na mama yake Alexandra. Wazazi wake walikufa akiwa mdogo .Akalelewa na ndugu, baadae akaolewa na Nebridius ambaye naye pia alikufa.

Mtakatifu Olyimpius alikataa kuolewa tena, akaamua kukabidhi maisha yake kwa Mungu, akilitumikia kanisa.
Mwaka 391 alikabidhiwa mali ambazo zilikuwa urithi wake, toka kwa wazazi wake.Na wakati huo, tayari alikuwa rafiki wa mtakatifu John Chrysostom ambaye alikuja kuwa Askofu wa Constantinople.
Mtakatifu Olyimpius alianzisha hospitali na kituo cha yatima.
Akasaidia watawa waliofukuzwa huko Nitria na pia akamsaidia Mtakatifu John Chrysostom alipofukuzwa  huko Constantinople. Akakosa kuwatii watawala ambao walikuwa na mtazamo tofauti , hali iliyosababisha naye afukuzwe toka Constantinople , ambako alienda uhamishoni Nicomedia (sehemu ya Uturuki) ambako alikufa tarehe 25 Julai mwaka 408.
Mt.OLYIMPIAS UTUOMBEE.





Mtakatifu Mary Di Rosa

Mtakatifu Mary Di Rosa alizaliwa mwaka 1813 Novemba 6, huko Brescia , Italia katika familia ya kitajiri.Alibatizwa Paolina Francesca di Rosa.

 Alipelekwa kusoma katika Convent ya masista wa Visitation .Akiwa na miaka17 mama yake alifariki.Ikamlazimu kuacha shule kusudi amsaidie baba yake katika kusimamia shughuli za nyumbani kwao.Akaanza pia kuwasaidia wasichana waliofanya kazi katika miradi ya baba yake.

Mwaka 1836 kulitokea mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Paolina Francesca di Rosa alifanya kazi katika hospitali ya mjini Brescia, akawa maarufu sana .

Akaanzisha nyumba ya kusaidia wasichana, akaanzisha nyingine maalum kwa wasichana viziwi na bubu.Mwaka 1840 akiwa na miaka 30 akawa mkuu wa jumuia ambayo baadae ilikuwa shirika. Akachukua jina la Mary Crocifissa di Rosa.Shirika liliitwa Handmaids of Charity.

Lilishughulika na kujali maskini , wagonjwa na wote wanaoteseka.Likazaa shirika jingine lililoitwa Servant of Charity. Hawa waliwauguza walioumia katika uwanda wa vita, kaskazini mwa Italia.Alipata moyo wa kufanya yote hayo, kwa kumuangalia Kristu , Msalabani.Papa aliwatambua rasmi mwaka 1850. 

Mtakatifu Mary Di Rosa alikufa mwaka 1855, Desemba 15 , Brescia, Italia.Alitangazwa mwenye heri, na mwaka 1954 akatangazwa mtakatifu na Papa Pius XII



Mtakatifu Ammon na wenzake Mashahidi
Mtakatifu Ammon na wenzake, Ptolemy, Theophilus na Zeno, walikuwa askari walinzi kutoka katika kikosi cha Theban ,katika jeshi la Warumi. 

Askari hawa waliamua kumfuata Kristo, na walipata mafundisho ya awali kutoka kwa Wamisri, ambao walikwisha kupata habari njema za Kristo, na kuamua kuwa wakristo. 

Lakini pia, askari hawa,walishuhudia wakristo wengi wakiuwawa katika kipindi cha mashtaki ya wakristo,  wakati wa utawala wa Decius. Walioana jinsi mashujaa wa imani walivyo kufa kwa mateso.Jambo hilo liliwapa nguvu ,kuungama imani yao hadharani.

Hiyo ilipelekea Ammon na wenzake kufungwa jela, na mwisho kuuwawa kwa kukatwa vichwa.     
MTAKATIFU AMMON UTUOMBEE.


Mtakatifu Yohane Mtume na mwinjili

Mtakatifu Yohane alizaliwa huko Bethsaida Galilaya katika karne ya kwanza. Alikuwa mwana wa Zebedayo na Salome.

Mtakatifu Yohane, alikuwa mmoja kati ya mitume 12 wa Yesu. Alikuwa pia na nduguye aliyeitwa Yakobo . Mtakatifu  Yohane na Yakobo pamoja na Petro walishuhudia Yesu akimfufua binti wa Yairo. 

Mtakatifu Yohane,  alikuwepo msalabani akiwa na mama Maria, wakati Bwana Yesu aliposulibishwa.

Baada ya Bwana kupaa mbinguni,Mtakatifu Yohane alienda katika nchi ya Waefeso na baadaye akaishi katika kisiwa cha Patmos ambako aliandika kitabu cha Ufunuo. 

Mtakatifu Yohane alikufa mwaka 100 (baada ya Kristo ), katika kisiwa cha Patmos, Ugiriki.

 MT YOHANE UTUOMBEE 




Mtakatifu Anastasia shahidi
Mtakatifu Anastasia alizaliwa katika karne ya 2 huko Roma.Baba yake aliitwa Praetextatus.Mtakatifu Anastasia alifundishwa na mtakatifu Chrysogunus.

Baadae mama yake Anastasia alikufa, na baba yake alimuozesha kwa mpagani aliyeitwa Publius.Lakini Mtakatifu Anastasia hakuwa tayari, aliamua kubaki bikira, akimtumikia Mungu.

Nyakati hizo za dhuluma kwa wakristo katika utawala wa Diocletian, wakristo wengi walikuwa katika magereza mbalimbali.Mtakatifu Anastasia aliwatembelea wafungwa hao, akiwasaidia katika mambo mbalimbali ya kiroho.

Mumewe alipogundua hilo alimfungia, akimpiga na kumtesa.Mwanaume Huyo ( Publius) alipokufa, Anastasia aligawa mali zake kwa maskini na wahitaji.Akawa anawasiliana na mtakatifu Chrysogonus ambaye muda huo alikuwa huko Aquileia (Italia).Huko Mtakatifu Chrysogonus alikamatwa na akahojiwa na Diocletian , aliyemtaka akane imani yake.Alipokataa alikatwa kichwa.

Muda huo pia kulikuwa na watawa watatu, Ambao ni Agape, Chione na Irene ambao walikuwa pamoja na mtakatifu Chrysogonus.Mtakatifu Anastasia alienda kuwafariji , na kuwapa nguvu.Lakini nao pia, walikamatwa ,wakateswa, na kuuwawa.Mtakatifu Anastasia aliwazika .

Mtakatifu Anastasia alizunguka miji mingi ,akiwasaidia na kuwapa moyo wakristu katika nyakati hizo ngumu.
Mtakatifu Anastasia alikamatwa huko Illyricum.Naye akalazimishwa akane imani yake.Alikataa.Kuhani wa kiapgani aliyeitwa Ulpian alijaribu kumgusa ,lakini alikufa muda mfupi baadae.Ikabidi aachiwe huru.

Mtakatifu Anastasia akisaidiana na mama mjane aliyeitwa Theodata, waliendelea kuwasaidia wakristu katika sehemu mbalimbali.Baadae tena Theodata naye akakamatwa akauwawa.

Mtakatifu Anastasia, alikamatwa tena,akahukumiwa kukaa jela siku 60 bila chakula.Alikaa siku hizo zote bila madhara.Ikaamuliwa awekwe katika boti iliyotoboka ili afe kwa kuzama.Lakini boti haikuzama .

Akachukuliwa na kupelekwa katika kisiwa cha Palmaria, ambako alichomwa moto hadi kufa.Hiyo ilitokea tarehe 25 Desemba katika karne ya tatu.

Utuombee.



Mtakatifu Thomas Becket,Askofu na Shahidi
Mtakatifu Thomas Becket alizaliwa mwaka 1119 Desemba 21, huko Cheapside, London, Uingereza. Alisoma masomo ya awali katika shule ya Merton Priory huko Sussex, na baadae chuo kikuu cha Paris.

Aliporudi London,alifanya kazi ya karani wa mahakama ,na alipofika miaka 24, alipewa kazi katika makazi ya Theobald, ambaye alikuwa Askofu mkuu wa Canterbury. 

Kwa ruhusa ya Askofu, mtakatifu Thomas alisoma sheria za kanisa katika chuo kikuu cha Bologna huko Hispania na kuendelea katika chuo kikuu cha Auxerre, huko Ufaransa. 

Mwaka 1154 alipata daraja la ushemasi, akitumika kama shemasi mkuu .Mwaka 1161 Askofu mkuu Theobald alikufa.Mwezi Mei mwaka 1162,Mtakatifu Thomas akachaguliwa kuwa Askofu,  akapewa kwanza daraja la upadri mwaka 1162 June 2, na  kesho yake June 3, akasimikwa kuwa Askofu  . Akawa Askofu wa Canterbury, japo alifahamu kuwa kwa kuzingatia misingi ya kanisa,  asingelewana na mtawala wa Uingereza wakati huo.

Na kutokana na misimamo yake thabiti ya kufuata taratibu za kanisa, akiwa kama Askofu,  alikosana na mfalme, na kukosa kukubaliana nae mambo mengi.

Mtakatifu Thomas Becket aliuwawa kanisani katika  cathedral ya Canterbury na askari waliotumwa na mfalme, mwaka 1170, Desemba 29, na akazikwa humo humo katika Cathedral ya Canterbury. 

Mtakatifu Thomas  Becket  alitangazwa mwenye heri mwaka 1173 February 21 na kutangazwa mtakatifu siku hiyo hiyo na Papa Alexander II


Mtakatifu Simeon wa Mnarani
Mtakatifu Simeon alizaliwa kati ya mwaka 390, Kozan (Uturuki sasa).Akiwa na miaka 13 tu, alianza kuchunga kondoo nyikani. Akiwa na miaka 18, siku moja alishindwa kuwapeleka malishoni kondoo, hivyo aliamua kwenda kanisani. Baada ya kumsikiliza mhubiri, aliamua kujiunga na  Manosteri iliyokuwa nje ya mjini,  iliyoongozwa na Abba John.

Huko alipokelewa na kuanza maisha ya utawa, na baadae mtakatifu Simeon aliomba kupanda na kukaa juu ya mnara uliokuwa hapo katika manosteri, akifunga
 na kusali.

Mtakatifu Simeon alikuwa na kipaji cha uponyaji, na umaarufu wake ukasambaa kila mahali. Watu walijazana mnarani, kutoka sehemu mbalimbali, wakiombewa.

Akajengewa mnara mwingine wa futi 40, ambako alikaa kwa muda mrefu. Kuna wakati Askofu wa Antiokia, alifika hapo, na kumwamuru mtakatifu Simeon kushuka.Alitii nakushuka .Alipewa daraja la ushemasi na kuendelea kukaa mnarani.

Mtakatifu Simeon alikufa akiwa na miaka 75, huko Qalaat Semaan, Byzantine  (kati ya Aleppo na Antiokia )



Mtakatifu Elizabeth Ann Seton  
Mtakatifu Elizabeth alizaliwa mwaka 1774 August 28 huko New York city. Mwaka 1794 aliolewa na William Magee Seton ambaye alikuwa mfanyabiashara.

Mume wake (William Seton )alifariki mwaka 1803, huko Italia. Na Mtakatifu Elizabeth alipoenda huko, ndipo  alipoamua kuwa mkatoliki.

Mtakatifu Elizabeth alirudi Marekani mwaka 1805, na kuanza maisha mapya, akiwa mjane, mkatoliki. Na mwaka 1809 aliamia Emmitsburg, Maryland ambako alianzisha shirika  (Charity of Saint Joseph ), ambalo lilikuwa la kwanza kwa watawa wanawake nchini Marekani.

Alianzisha pia shule (St Joseph academic )ambayo walisomesha watoto maskini bure.Shule hiyo ikawa chachu kwa elimu katika jamii za wakatoliki, na kusaidia wasioweza kumudu gharama za shule.

Mtakatifu Elizabeth Ann Seton alikufa mwaka 1821, Januari 4 huko Emmitsburg, Maryland Marekani. 

Alitangazwa mwenye heri mwaka 1963 March 17 na Papa John XXIII, na akatangazwa mtakatifu mwaka 1975 Sept 14 ,na Papa Paul VI.


*JE WAJUA MAANA YA NENO "IHS" LILILOKO KWENYE VAZI LA PADRE?*

• Iko hivi...

Wengi tumekuwa tukishangaa mavazi ya Mapadre, vitambaa na vitu mbalimbali vya Ibada kuwa na alama hiyo, kama ilivyo kwenye hiyo picha hapo chini.

Leo nataka nikujuze kidogo maana yake na historia yake, hivyo nakusihi ujitahidi usome mpaka mwisho.

Maneno yasiwe mengi. "IHS" ni ufupisho wa Jina Takatifu la Yesu kwa Kigiriki *"IΗΣΟΥΣ"* na imeanza kutumika tangu karne ya pili mpaka leo karne ya 21.

Kwani kabla kipindi cha Wakristo kuteswa na kuuawa na utawala wa kidhalimu wa Kirumi, maandishi hayo yalitumiwa kama alama ya siri *(secret code)* katika nyumba, makaburi na Makanisa ya siri ya Wakristo. Nao Wakristo wakiiona, iliwarahisishia kujua kuwa hapo ndio kwao.

Mtakatifu Bernadine wa Siena (1380-1444) na Mwanafunzi wake Mtakatifu Yohane wa Capistrano (1386-1456) walitumia alama hiyo kueneza Ibada ya Jina Takatifu la Yesu.

Miujiza mingi sana ilitendeka kupitia alama hiyo, hadi kuwafanya watu wengine kuhisi kuwa ni ushirikina. Ndipo mnamo mwaka 1427, Papa Martin V alipopitisha Ibada hii na akaelekeza iwekwe pia na Msalaba katikati yake, kama ilivyo kwenye hiyo picha hapo chini.

Watu wakashangaa inawezekanaje Jina kuponya? Yesu mwenyewe aliahidi hili: "Kwa Jina langu watatoa pepo, na kusema kwa lugha mpya. Wakishika nyoka au wakinywa kitu chochote chenye sumu, hakitawadhuru. Watawekea wagonjwa mikono, nao watapona" *(Marko 16:17-18).*

*Pia ukipata muda, soma Mdo 2:21, Mt 4:1-11, Yoh 16:23-24 na Kol 3:17.*

Lakini kutokana na kufifia kwa lugha ya Kigiriki duniani, na lugha ya Kilatini kushamiri, ndipo alama hiyo ya *"IHS"* ikatafsiriwa kama "Iesus Hominum Salvator" yaani "Yesu Mwokozi wa wanadamu" bila kupoteza maana yake ile ile ya mwanzo.

Kumbuka alama hiyo ipo kwa ajili ya kutangaza tu Ukuu wa Jina Takatifu la Yesu, na sio vingenevyo.

*...TUMSIFU YESU KRISTO...*


Mtakatifu Anysia Bikira na Shahidi
Mtakatifu Anysia alizaliwa huko Solanika, Thessaly, Ugiriki, katika familia ya kikristo. 

Aliamua kuweka wakfu maisha yake, kuishi maisha safi na ya kimaskini , akisali na kusaidia maskini.

Lakini nyakati hizo zilikuwa nyakati za madhulumu kwa wakristo, chini ya utawala wa mfalme mpagani Maximian ambaye alikuwa Mrumi. 

Mwaka 304, alitoka kwenda kanisani, na njiani akakutana na askari wa Kirumi.Askari huyo alipogundua kuwa Anysia ni mkristo,  alianza kumpiga na alitaka kumpeleka katika hekalu la kipagani ,amtoe sadaka. 

Alipomchania ushungi wake, kwa kumdhalilisha, mtakatifu Anysia alimtemea mate usoni. Askari huyu, alimchoma na upanga, ambao ulitokeza mpaka upande wa pili, na kumuua.      




JINA TAKATIFU LA YESU.

Umeshawahi  kutafakari juu ya jina Takatifu la Yesu. Tujiulize   jina hilo takatifu lilitoka wapi?Tena lina nguvu za ajabu maana kwa jina hili watu wanapona,wanatakaswa,wanazaliwa upya, jina hili ulisharitafakari hata kidogo:

Katika Injili ya Mathayo 1:20-21, tumeona kuwa Malaika Gabriel alivyomtokea mtakatifu Yosefu, akimwambia habari ya kuzaliwa kwa mtoto Yesu na jina lake. Pia alimwambia maana ya jina hilo. Katika maelezo yake Malaika alisema; *"Naye atazaa mwana, nawe utamuita jina lake Yesu.* *Maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao".* 

Na katika kitabu cha Matendo ya mitume, 4:12, tunasoma, *"Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote,  kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu,  walilopewa  wanadamu  litupasalo sisi  kuokolewa kwalo.*

Jina la Yesu linatupa uhuru kamili, kwa kuwa kwa jina hilo, tumekombolewa.

Bwana Yesu kwa nguvu ya jina lako tujiliye kushiriki uzima wa milele.Amina.




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUSALI ROSARI TAKATIFU YA BIKRA MARIA

MALAIKA MKUU MT. MICHAEL UTULINDE KATIKA VITA

ROZARI YA KUWAOMBEA MAREHEMU TOHARANI

SALA KWA AJILI YA KUFUNGULIWA KUTOKA KATIKA NGUVU ZA GIZA

HISTORIA YA MAISHA YA BIKIRA MARIA

FAHAMU JINSI YA KUOMBA SALA YA VITA