HADITHI YA KWELI KUHUSU MAREHEMU WALIOKO TOHARANI
HADITHI YA KWELI KUHUSU MAREHEMU WALIOKO TOHARANI.
Siku moja huko San Giovanni Rotondo, Padre Pio pamoja na Watawa
wenzake walikuwa wanasali, mara walisikia sauti za ajabu zikitoka kwa Kasisi.
Mmoja wa Mafrateli alisikika akisema:
"Tulisikia sauti za ajabu huku zikiwa zinaimba kwa
mtiririko mzuri, lakini cha kushangaza hakuna aliyejua chanzo cha sauti hizo
zilikuwa ni nini".
Wakati hayo yakiendelea, Padre Pio alikuwa amezama sana katika
maombi, ndipo Mtawa mmoja akamkaribia ili kumuuliza kama kweli anajua uimbaji
huo ulikuwa unatoka wapi.
Wakati alipomgusa, Padre Pio alishtuka kana kwamba ametoka
katika usingizi mzito sana, kisha akajibu:
"Mbona nyote mmeshangaa? Hizo mnazozisikia ni sauti za
Malaika zikiimba, huku wakizitoa roho kutoka Toharani na kuzipeleka
Mbinguni".
Padre Pio hakuweza tu kusikia, bali pia aliweza kuona kwa macho
ya rohoni kila kitu kilichokuwa kinatendeka muda ule.
Pia nyakati zingine, alipewa zawadi ya kujua hali ya milele kwa
wale wanaokufa. Na inasemekana kwamba:
Siku moja alitembelewa na Mjane mmoja ambaye Mume wake alijiua,
aliyemuuliza kuhusu roho ya Mume wake na Padre Pio akamjibu:
"Ukweli Mume wako ameokoka, kati ya daraja na moto
alimojitupa, kwa kuwa alitubu".
Basi zawadi za Padre Pio zisizokuwa za kawaida, hazikuja kwa
urahisi. Daima alitambua maisha yake ya mateso makali, ikiwemo kubeba Majeraha
ya Stigmata (yaani Madonda ya Yesu) kwa zaidi ya miaka 50, kwa ajili ya
marehemu Toharani.
Katika mateso yake, Padre Pio alikuwa na Ibada maalumu kwa roho
zilizomo Toharani. Mapema katika Ukuhani wake, alimwandikia Mkurugenzi wake wa
kiroho kuwa:
"Tamaa hii imekua mara kwa mara moyoni mwangu, hadi sasa
nimekuwa na shauku kubwa kwa ajili ya hiyo.
Kwani nilitoa dhabihu hii kwa Bwana, nikimsihi aniweke juu yangu
adhabu ambazo zimetayarishwa kwa ajili ya wenye dhambi na roho zilizomo
Toharani, na kuzidisha juu yangu adhabu hizo hata mara mia, Ili roho yenye dhambi
ikoke na kuachilia haraka roho zinazoteseka Toharani".
Padre anaendelea kusema kwamba:
"Mateso yalipozidi bila faraja, ilikuwa furaha yake kubwa,
kwa sababu yaliyafanya maumivu ya Yesu kuwa mepesi".
Basi ndugu zangu, kesho tunapojiandaa kushiriki sherehe ya
Kristo Mfalme, tusisahau kuwaombea ndugu zetu marehemu walioko Toharani.
Kwani Bwana Yesu mwenyewe aliahidi kwamba: "Katika sherehe
hii, yeyote atakayesali kwa ajili ya kuwaombea marehemu wake, basi atazifungua
roho hizo kutoka kwenye kifungo cha mateso na kuwaingiza katika Ufalme wake wa
milele, kama tu mtu huyo atasali kwa imani na kupokea Ekaristi Takatifu."
*RAHA YA MILELE UWAPE EE BWANA...*
Maoni
Chapisha Maoni