NGUVU YA SALA ALIZOFUNDISHWA MTOTO GRACE
NGUVU YA SALA ALIZOFUNDISHWA MTOTO GRACE
UTANGULIZI
Sala hizi ni sala zilizoandikwa
na mtoto Grace mwenyewe, akiongozwa na Mt. Michael Malaika Mkuu, na sala hizi
ziliandikwa baada ya ombi maalum toka kwangu, hii ni baada ya kutaka kudadisi
Malaika wanamfundisha nini mtoto Grace awapo usingizini, maana wakati mwingine mtoto
Grace akiwa kalala na ukienda kumwamsha kama nafsi yake haipo hapo, alinyoosha
mkono tu kutoa ishara ya kusubiri, basi tuliweza kusubiri mpaka alipozindika
peke yake.
Hata pale alipoweza kuamka
ulipomuuliza alikuwa wapi, naye alijibu wakati umekuja kuniamsha, Mt. Michael
Malaika Mkuu alikuwa ananifundisha sala, au anaweza kukujulisha alikuwa na
Malaika Enjo au Anjelina hawa ni Malaka waliojitambulisha kwa Majina hayo ndani
ya familia, basi baada ya kugundua kuna kitu kinaendelea, ndipo nilipomwomba
mtoto Grace aweze kuandika sala zote anazofundishwa na Malaika.
Mt. Malaika Michael siku moja
alikuja na kuongea nami na kusema, mtoto Grace ataweza kuandika sala baadhi tu,
msimlazimishe kuandika sala zote maana kuna sala zingine zina nguvu sana na
endapo ataziandika nyinyi binadamu mnaweza kuzisali kawaida bila kujiandaa na
kutokujua nguvu ya matokeo ya sala hizo, hivyo sitatoa kibali cha uandishi wa sala
hizo ambazo zitabaki kuwa ni sala za mtoto Grace ambazo anaweza kuzitumia yeye
tu katika ulimwengu wa roho.
Baada ya maelezo hayo sikuwa na
namna yeyote zaidi ya kuwa mtii, ndipo nilipoambulia sala hizi ambazo leo
nakushirikisha nawe, kuzisali, sali kwa imani na kumaanisha hakika utaona
huruma ya Mungu na Upendo wake wa ajabu juu yetu sisi wanadamu. Karibu tusali
pamoja Amina.
Shukrani
Napenda kutoa shukrani za dhati
kwa Mwenyezi Mungu muumba mbingu na nchi kunitia nguvu kuweza kutengeneza
kitabu hiki kidogo cha sala.
Natoa shukrani kwa mtoto Grace
katika uandishi wa sala hizi.
Na kwa umuhimu nimshukuru Mt.
Michael Malaika Mkuu kuwa pamoja nasi kwa ukaribu wa pekee, na kushiriki kwa
namna ya pekee kumfundisha mtoto Grace sala nyingi za vita vya kiroho na
kuifanya familia kuwa na Amani na leo kufanikisha kitabu hiki kidogo cha sala
ambapo ni kati ya mfululizo wa vitabu vinavyomgusa mtoto Grace ikiwa ni toleo
la tatu.
Nawashukuru ndugu zangu, ambao
wamekuwa wafadhili wakubwa wa familia yangu, pia namshukuru mke wangu ambaye
amekuwa kiongozi bora wa Imani ndani ya familia.
Mwisho nikushukuru wewe msomaji
ambaye umeguswa na kitabu hiki, Mungu Mwenyezi Muumba mbingu na nchi azidi
kukutia nguvu katika maisha safi ya kiroho Amina.
1.
SALA
YA KUVUNJA MADHABAHU ZA KICHAWI
Mungu Baba Mwenyezi uliyeumba
mbingu na dunia tunakushukuru kwa kutuweka duniani na kutupatia nguvu, Ee Mungu
tunaomba utupe nguvu za kukutumikia wewe, sisi tumekosa sana tunaomba msamaha
kwa dhambi zetu, Ee Mwenyezi Mungu kuna binadamu wanaojenga madhabahu kinyume
kabisa na mapenzi yako, tunaomba nguvu sasa na tunakwenda kinyume na madhabahu
za kichawi popote pale zilipo iwe kwenye bahari ninaziteketeza kwa jina la Yesu
Kristu wa Nazarethi, roho Mtakatifu tunaomba ututangulie kwa jina la Yesu
Kristu, Mungu Baba Mwenyezi tunaomba utupe nguvu za kubomoa nguvu za kichawi,
popote zilipo, na madhabahu zake zote tunaomba nguvu ya afya ya roho na mwili –
Amina.
2.
SALA
YA KUVUNJA VIOO (SCREEN) NA MAPEPO YANAYOZUIA MAOMBI
Ee Mungu tunakwenda kinyume dhidi
ya mapepo yote yanayozuia maombi, tunakwenda kinyume dhidi ya screen za kipepo,
za kichawi za majini zinazotumika kuangalia watu wa Mungu, tunapofua macho yenu
ninyi mapepo mnaoshika maombi ya watu wa Mungu, tunakatakata mabawa yenu
kuanzia sasa na kila pepo arukaye, kila pepo ashirikiaye maombi, Ee Mungu
tunaomba umtume Malaika Michael akawateketeze kwa upanga wako Mtakatifu,
tunaomba utujalie nguvu shetani asipate nafasi juu yetu, juu ya watu wote wa
Mungu Amina.
- Mtakatifu
Michael Malaika Mkuu- utulinde na kutuokoa. Amina
3.
SALA
YA KUOMBEA WATOTO WANAOTOLEWA MIMBA
Ee Mungu tunakushukuru kwa afya
njema, tunaomba Mungu kwa msaada wako na kwa nguvu zako za ajabu uliumba watoto
na ukasema watoto wadogo wote waje kwako, ila kwa kuwa sisi binadamu hatukutii,
sisi tumefanya isivyo kabisa.
Ee Mungu
tunaomba msamaha kwa ajili ya hili tatizo la utoaji mimba, Ee Mungu tazama
dunia ya sasa inapoelekea sio kuzuri, tunaomba msaada wa maombezi ya mama Bikra
Maria, mama yetu, mama wa Kanisa, mama wa watoto yatima, mama wa watoto
wanaotolewa mimba.
Tunajua
hili ni chukizo mbele za Mungu na kwa mama yetu Bikra Maria, tunaomba kwa uwezo
wako Mungu uwashushie huruma wakina mama, mabinti wa sasa na kizazi kipya hata
kijacho huruma yako, wajue kwamba utoaji wa mimba haukupendezi wewe Mungu wetu
unakuchukiza, pia waonee huruma kwa viumbe hivyo wanavyohitaji kivikatiza
maisha, kuvihukumu bila makosa kwa maana watoto hao ni watoto wa Mwenyezi Mungu
hawana makosa.
Ee
Mungu wape watu wote wanaohitaji kutoa mimba huruma na wajue ya kwamba watoto
hao pia wanahitaji kuishi kama wenyewe wanavyoishi na pia wakuogope wewe Mungu
uliye waumba na kuwapatia uhai, tunajua sisi wanadamu hatuna mamlaka ya kutoa
uhai wa mtu mwingine isipokuwa wewe tu, hivyo basi tunaomba msaada wako,
uwajalie binadamu huruma na wajue hawana mamlaka ya kutoa uhai wa mtu mwingine.
Tunaomba hayo yote kwa njia ya Kristu – Amina.S
Bikra Maria mama wa watoto x 3
tuombee
Bikra Maria mama wa msaada wa dunia
utuombee x 3
Salamu Maria x 3
4.
SALA
YA KUOMBA ULINZI WA MALAIKA
Ee Mungu Mwenyezi uliyeumba
binadamu na Malaika tunakushukuru kwa kuweza kuumba vitu vyote vinavyoonekana
na visivyoonekana, kwa nguvu na uwezo wako wa ajabu ulimuumba binadamu na kila binadamu
ulimpatia Malaika walinzi na sisi pia hatunabudi kuwaheshimu, tunaomba uwatume
Malaika wako waje watulinde katika hatari zote za roho na za mwili, tunaomba
Malaika wako watulinde, watuongoze sehemu ya kupita siku zote za maisha yetu,
tunaomba enyi Malaika ulinzi wenu uwe pamoja nasi, msituache katika matope,
mtufundishe jinsi ya kusali, jinsi ya kumheshimu Mungu wetu Amina.
- Enyi
Malaika wetu Watakatifu - mtuombee x 3
- Enye
Malaika walinzi wetu – mtuombee x3
5.
SALA
YA KUOMBEA FAMILIA
Ee Mungu Baba Mwenyezi,
tunakushukuru kwa kuweka familia, ukaweka baba, mama na watoto na pia ukamfanya
baba kuwa kichwa cha familia na ukampa mamlaka ya kuongoza familia, tunaomba
huruma yako ishuke katika familia zetu, weka amani katika familia, weka upendo,
furaha na kuweza kuheshimiana sisi wenyewe kwa wenyewe, mpe nguvu baba wa
familia, ondoa nguvu yoyote inayomfanya kutokujua wajibu wake kama baba wa
familia, pia wabariki watoto uwajalie heshima kwa wazazi wao, unyenyekevu kwa
wazazi wao, Ee Mwenyezi Mungu tunaomba ulete amani kwenye familia zenye
mfarakano, familia zisizokuwa na amani, upendo, furaha, familia zenye vurugu
ukarudishe amani, upendo Amina.
Mama wa familia Takatifu utuombee
x 3
6.
SALA
YA KUOMBEA MAPADRI NA WATAWA
Ee Mungu baba Mwenyezi
tunakushukuru kwa afya ya roho nay a mwili, pia tunashukuru kwa ajili ya
kulipatia Kanisa lako Mapadri na Watawa. Mapadri hao wanayo nguvu ya kugeuza
mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristu, Mapadri hao wanao wajibu mkubwa wa roho
zetu, Ee Mungu tunaomba ulipatie Kanisa lako Mapadri walio watakatifu wa
kulitumikia Kanisa lako takatifu na pia tunaomba uwajalie Mapadri na Watawa
moyo wa uvumilivu, wakutangaze wewe na kukuheshimu, tunaomba uwajaliye moyo wa
unyenyekevu, amani, upendo, furaha, uwajalie waweze kushinda hila zote za
shetani, wape nguvu ya kulitangaza neno lako pasipo woga wowote na mwisho
waweza kushinda hila za yule mwovu, kwa maombezi ya Bikra Maria Rosa mystica
aweza kuwaombea Mapadri na Watawa wote. Awape moyo wa kuvumilia majaribu yote
watakayokumbana nayo. Amina.
Ee Mungu mwenye huruma twakuomba
uwajaze nguvu mioyo yao, isiweze kuwa baridi na pia waweza kutimiza ahadi
waliyoiweka kwako katika madhabahu yako mpaka kufa kwao, waweze kuishi maisha
ya usafi wa moyo – Amina.
Maria Rosa mystica utuombee x 3
Wote, waweza kuishi maisha ya
kumpendeza Mungu utuombee x 3
Baba yetu x 3, salamu maria x 3,
atukuzwe x
7.
SALA
YA KUOMBEA MATAIFA
Ee Mwenyezi Mungu Muumba Mbingu
na dunia kwa uwezo wako wa ajabu, uliumba binadamu wakujue wewe, wakutumikie
wewe, lakini hawafanyi hivyo, tunaomba ushushe mkono wako wa Baraka katika
Mataifa yote, leta amani, upendo na furaha katika Mataifa yote tunakuomba
ukayabadirishe Mataifa yanayomwaga damu, hayana amani wala furaha na uyaletee
amani na furaha ili kusudi mwovu asipate nafasi katika Mataifa hayo, Mungu
Mwenyezi tunajua kwamba wewe pekee ndiye uliyetupatia uhai, wala si mwingine na
wewe ndio mwenye uwezo wa kutoa uhai wa mtu.
Tunaomba kwa maombezi ya Bikra
mama wa msaada, mama wa neema zote tunaomba uyalinde Mataifa yote uzuie vita na
pia ulete amani katika Mataifa yote, tunajua ya kwamba pasipo neema ya Mungu
hatuwezi chochote hivyo basi tunaomba amani kwa Mataifa yote yenye kukuabudu,
yenye kukuheshimu na hata yenye kukudharau,na yenye kukufuru wewe Mungu,
tunaomba hasira yako isitushukie sisi wanao japo tunajua tumekukosea wewe,
tunaomba msamaha kwa yote tuliyo yafanya ambayo hayakupendezi wewe, pia
tunaomba msaada wa Bikra Maria mama yetu, mama wa Mataifa, mama wa watoto wote,
Ee Mungu tunaomba huruma yako itukinge na hila zote za yule mwovu shetani na
mwovu asipate nafasi ya kutudhuru.
Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu
Kristu wa Nazareti – Amina
Bikra Maria msaada wa daima
utuombee x 3
Bikra Maria wa neema utuombee x 3
Salamu maria x 3
8.
SALA YA
KUMFUNGA ADUI YEYOTE ANAYEINGILIA MAISHA YAKO
Ninamfunga mwovu anayenisumbua
katika maisha yangu na ukoo wangu, ninamfunga na mamlaka yake, ufahamu wake wa
kichawi, vitu anavyotumia visipate kurudi tena na mwisho akaombe msamaha,
katika jina la Yesu Kristo naomba.Amina
9.
SALA YA KUJIKINGA NA MUOVU
Ewe Roho Mtakatifu tunaomba
utukinga na muovu yoyote, akija akutane na damu ya Yesu, nayo imemchome
atakaporudi damu hii ikaendelee kumchoma mpaka kwenye kiti anachokaa na vitu
vyake na washiriki wake wakateketee wote. Amina.
10. SALA YA KUVUNJA LAANA ZA UCHAWI (03/07/2015)
Anza na kusali sala ya Mt. Michael,
ninawafunga na kuvunja nguvu zenu wachawi wote na sorcerer wote wanaofuatilia
maisha yangu kwa namna yeyote ile.
Kwa nguvu ya kusulubiwa na damu ya
Yesu Kristo iliyomwagika msalabani, ninasambaratisha njia zote za kipepo
(sprit-guides) wa wachawi na waabudu mizimu, Roho za wahenga zilizofutilia
maisha yangu kwa njia ya nguvu zao za kichawi ili kuweza kunidhulu, kwa jina la
Yesu ninawasambaratisha. Amina.
11. JIWEKE HURU NA MAAMBUKIZO YA KICHAWI
- Sali kwanza
sala ya Mt. Michael (inayojulikana)
- Mungu baba
nakushukuru kwa damu ya Yesu Kristo mwano mpendwa, leo nakuja kwako kwa neema
yako uniweke huru kutokana na kile ambacho nimeambukizwa mwilini kwa njia ya
Roho.
Nasalimisha kila mbegu ya kichawi
iliyopandwa ndani yangu naomba damu ya mwanakondoo inisafishe, pia kila
ambukizo lolote ambalo limeitishwa ndani yangu wakati ningali tumboni mwa mama
yangu, nalisambaratisha ambukizo hilo kwa jina la Yesu na lisipate nafasi tena
kwangu kwa jina la Yesu. Amina.
12. MAOMBI YA VITA DHIDI YA MAADUI WANAOJIFICHA
KWENYE MWAMVULI WA MASWALA YA MUNGU.
(Wale wanaovaa mavazi ya kondoo
hali ndani ni fisi) 04/08/2015
Kwa maombezi ya Bikra Maria
Mtakatifu na watakatifu, Ee Mungu baba ninaomba utume Roho Mtakatifu aweze
kumfichua mchana kweupe shetani yule ambaye amejificha kwenye mwamvuli wa dini
hali ndani ni fisi, kwa jina la Yesu ninamfunga ili asipate kurudi tena. Amina
13. SALA DHIDI YA MAPEPO WAHARIBIFU NA MAUAJI
(05/8/2015)
Ee Mungu ninamfunga shetani
mwaribifu na muuaji naanzisha mapambano dhidi ya uharibifu waliotumwa na
shetani kuharibu mali zangu, Baba, imeandikwa katika Yer 51:25 “mimi
ninapingana nawe ewe mlima mharibifu, mlima unaoharibu dunia nzima! Nasema mimi
mwenyezi Mungu. Nitanyoosha mkono wangu dhidi yako, nitakuangusha kutoka
mwambani juu ya kukufanya kuwa mlima uliochomwa moto” Baba niepushe na njia za
Yule muovu anayenisumbua na ukamfunge shetani daima kwa jina la Yesu Kristo,
Amina.
14. SALA YA KUJIKINGA NA MAOVU (06/8/2015)
Ee Yesu mwema ninaomba unikinge na
maadui wowote wanaonizunguka, wateketeze na nguvu zao zote ambazo ninaziweka
chini ya Ekarist Takatifu / chini ya msalaba wa Yesu, Amina.
15. SALA YA KUMFUNGA SHETANI (07/8/2015)
Ninamfunga mwovu anayenisumbua
katika maisha yangu na ukoo wangu, ninamfunga na mamlaka yake yote, ufahamu
wake wa kichawi naufunga na ninauweka chini ya msalaba Mtakatifu wa Yesu Kristo
na vitu vyote vya kichawi visirudi tena na mwisho wakagombane wenyewe kwa
wenyewe na kuomba msamaha katika jina la Yesu, Amina.
16. SALA YA UPONYAJI KATIKA JAMBO KUBWA
Wewe Mungu hukichukii kitu chochote
ulichoumba bali wakipenda na kukistawisha, na kusihi uje hima kunisaidia katika
jambo hili, Ee Bwana wewe ni pekee msaada wangu na kimbilio langu, wewe unajua
namna unavyolishughulikia tatizo langu hili (taja tatizo) kama ni ugonjwa /
msiba unaokusumbua. Ee Mungu Mwenyezi pokea maombi niliyokutolea ili kwa neema
zako tuweze kuyapata kweli, Amina.
17. SALA YA KUJIKABIDHI KWA YESU
Ee Yesu naomba uwe pamoja nami
katika hatari zote za Roho na mwili na ninajikabidhi Yesu mikononi mwako,
lakini daima tuna matumaini makubwa katika wema na huruma yako takatifu, Amina.
Sala hii ya kujikabidhi kwa Yesu
ilisisitizwa kusali mara kwa mara na hasa utakapokuwa unatoka nyumbani, hivyo
kama familia sala hii tumekuwa tukisali kila siku yaweza kuwa zaidi ya mara
moja, kadri Mungu alivyotubariki siku hiyo Amina.
18. SALA YA KUMFUKUZA SHETANI, JINI KAHABA
(Anayechukua watoto duniani)
(15/10/2015)
Wewe jini kahaba kwa uwezo wa Mungu
Mwenyezi ninakuamuru na kuvunjavunja silaha zako zote unazotumia kubeba watoto
hapo duniani, ninaziharibu silaha hizo zote, ninakufunga wewe na mawakala wako
wote, ninaamuru, mizimu, wachawi, rusifeli, mapepo, majini kuwaachia watoto
wote, mabinti na nafsi za watu mlizozichukua ninawaamuru katika jina la Yesu
muwarudishe ulimwenguni Amina.
19. SALA YA KUOMBEA NDUGU, JAMAA NA MARAFIKI
WALIOTEKWA NA SHETANI
Baba Mungu Mwenyezi, ukawakomboe
watu wako waliotekwa na shetani katika jina la Yesu Kristo, maana hao ni watu
wako Mungu. Ninakuambia wewe shetani hauna mamlaka ya kuwashika watu wa Mungu,
waachilie katika jina la Yesu Kristu na ninawakabidhi watoto wako Yesu mikono
mwako, Amina.
20. SALA ZA KUVUNJA MAPEPO, MAJINI, VINYAMKELA NA
KIKARAGOSI VINAVYOCHUKUWA VITU HAPA DUNIANI KAMA KUCHA, NYWELE, VIDOLE NA NYOTA
YA MTU.
Baba ninavunja vunja nguvu za hawa
viumbe ambao wanasoma nyota za watu wa Mungu, Baba ukawatume Malaika wako wa
vita ili kuwateketeza hawa viumbe, Baba Mungu Mwenyezi ninaziharibu nguvu za
hawa viumbe wanaochukua kucha, nyota, nywele, vidole, ulimi na ukateketeze
miungu yao na hasa katika hiki kipindi kinachoendelea mpaka sasa, ninavunja
ngome zao zote zilizoko Magharibi, Kaskazini, Mashariki na Kusini na
kuziteketeza ngome hizo kwa moto wa Roho Mtakatifu, kwa jina la Yesu Kristo wa
nazareti Amina.
Hizi ni baadhi ya sala chache
alizoweza kuandika mtoto Grace ikiwa ni sehemu ya sala alizofundishwa na Mt.
Michael Malaika Mkuu, na hasa alisisitiza wakristo wajenge tabia ya kabariki
vitu wanapovinunua maana amegundua ujanja wa shetani, na kwa kubariki vitu
vyetu tutakuwa tumefaulu kuvunja hila za shetani.
Japo sala hizi ni fupi Sali kwa
imani sala utakayoichagua kila siku na kila mara. Na Mungu atakujibu.
N.B Tutafurahi kupokea ushuhuda
wako kupitia sala hizi.
©Imeandaliwa na:
Mtumishi: Julius Mmbaga
0766500747.
Maoni
Chapisha Maoni